HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro kwa mara ya kwanza tangu ilipoanzishwa inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Kituo cha kisasa cha Afya Tungi kitakachogharimu kiasi cha Sh bilioni 1.2 , fedha zinazotokana na mapato yake ya ndani.
Kituo hicho cha afya kitakachokuwa na huduma zote muhimu za afya kitahudumia watu takribani 16,793 wanaoishi Kata ya Tungi na nyingine za jirani katika Manispaa ya Morogoro .
Mkurugenzi wa Manispaa Ndg. Ally Machela amesema hayo wakati akizingumza na waandishi wa habari waliotembelea kujionea shughuli za ujenzi wa kituo hicho eneo la kata ya Tungi.
Machela alisema kituo hicho kinajengwa kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya na kina majengo 10 ya kutolea huduma mbalimbali kwa wananchi na kwa hatua ya kwanza ujenzi wake umetumia Sh milioni 350 ,fedha zinazotokana na makusanyo ya mapato ya ndani.
“ Kwa sasa tupo katika hatua ya upauaji na tayari tumelipa fedha Sh milioni 83 za ununuaji wa bati na bati hizo wametuahidi wiki ijayo kiwanda kitaleta hizo bati “ amesema Machela
Alisema mradi huo wa ujenzi katika kata ya Tungi umekuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wake na wengine wa kata za jirani kupata huduma za afya eneo la karibu .
“ Malengo ya Manispaa yalikuwa ni kujenga kituo cha afya ambacho kimetimia na kwa ujumla tumekidhi vigezo vyote vya majengo yote yanayotakiwa kwa ajili ya mradi wa afya” alisema Machela.
Mkurugenzi wa Manispaa alisema uamuzi huo ni kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ya kwamba huduma za afya zinafanyika katika kiwango ambacho ni timilifu kwa upatikanaji wa huduma zote muhimu kwa asilimia 100.
“ Ujenzi huu unafanyika kwa fedha za mapato ya ndani ,na Manispaa imeamua kwa makusudi kuhakikisha ya kwamba tuna kuwa na mradi mkubwa unaotokana na mapato ya ndani tuna miradi mingi ya mapato ya ndani lakini huu ni mahususi kwa ajili ya kituo cha afya na mahususi katika sekta ya afya “ alisema Machela
Machela alisema majengo hayo yatawekewa njia maalumu za kupita wagonjwa na watoaji wa huduma katika Kituo hicho .
Machela pia alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 , Halmashauri imetenga fedha za kumalizia Zahanati nne zilizopo kata ya Kingo , Kauzeni, Mkundi na Mazimbu na ndani ya miaka miwili , Manispaa itakuwa na zahanati zaidi ya 10 zilizokamilika na zinazotoa huduma.
Naye Mganga mkuu wa Manispaa Charles Mkombachepa alisema kituo hicho cha afya cha kisasa kina majengo hayo 10 ya kutolea huduma ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la akina mama wajawazito, jengo la maabara ,jengo la upasuaji akina mama wajawazito, jengo la akina mama wajawazito wanaojifungua na wenye shida mbalimbali za uzazi .
Mganga mkuu wa Manispaa pia alisema kituo hicho cha afya kina nyumba moja ya mtumishi , jengo la kufulia nguo pamoja na jengo la kuhifadhia maiti .
Nao wakazi wa Kata hiyo akiwemo Leticia Lukanima ameipongeza Manispaa kwa kujenga kwanza Zahanati katika eneo hilo inayowasidia kupata huduma za afya wakiwa karibu tofauti na miaka ya nyuma wakizifuata umbali wa kilometa tano kwenye kata nyingine ya Kichangani kabla ya kuanza mradi huo mkubwa wa kituo cha afya .
“ Tunampongeza Rais wetu kwa kutusogezea huduma hapa Tungi , tunapata huduma nzuri kutoka kwa wauguzi na madaktari na tunaangalia majengo mengine yanayojengwa ya kituo cha afya kikikamilika kitaboresha huduma zaidi na kutuondolea kufuata vipimo vya afya vituo vya mbali “ alisema Leticia
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa