MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Mhe. Norah Mzeru, ametimiza ahadi yake ya kukabidhi Mifuko 100 ya Saruji Shule ya Sekondari Lupanga iliyopo Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ambayo yameonekana kuchakaa.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Mzeru, Katibu wa Mbunge huyo , Ismail Kifaru, amesema kuwa mifuko aliyotoa Mhe. Mzeru ametumia fedha zake binafsi kununua mifuko hiyo lengo likiwa ni kusaidia kufanikisha ukarabati wa madarasa ambayo yameonekana kuchakaa ili yaendane na madarasa mapya na wanafunzi wasome katika mazingira rafiki yenye kuvutia.
Kifaru, amewataka wanafunzi wa shule ya Lupanga kusoma kwa bidiii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na atakuwa mstari wa mbele kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazo wakabili kwa kadri watakavyoweza kujaliwa.
Katika hatua nyingine, Kifaru, amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri pamoja na kushukuru waalimu kwa kujitoa kwao katika kufundisha na kuongeza ufaulu shuleni hapo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Afisa Taaluma Sekondari Manispaa ya Morogoro, Muhaiki Deogradia, amempongeza Mhe. Mzeru kwa mifuko hiyo ya saruji na kumuahidi mifuko hiyo itaenda kufanya kazi tarajiwa.
Naye Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, amemshukuru Mhe. Mzeru na huku akisema kuwa kitendo cha Mhe. mzeru kutoa mifuko hiyo ya saruji kinaonesha ni jinsi gani Mhe. Mzeru anaunga mkono Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassani ya kujenga miundo mbinu bora ya elimu na kuwezesha wanafunzi kusoma bila shida.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Lupanga, Flora Ndunguru, amesema kuwa Msaada huo utasaidia kutatua changamoto waliyo nayo ya uchakavu wa madarasa .
Amesema wanatarajia kupokea wanafunzi 274 , hivyo kwa madarasa ambayo watayakarabati basi yatasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.
Kwa upande wa mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliye jitambulisha kwa jina la Theresia Minja, ametoa pongezi kwa Rais Samia na kumshukuru Mbunge Mzeru , kwa moyo alioonyesha kujitoa kuwasaidia kutatua changamoto hiyo na kumuahidi kuwa watasoma kwa bidii na Kufaulu kwa asilimia 100 katika mitihani yao pamoja na kuongeza ufaulu shuleni hapo.
Ikumbukwe ahadi ya Mhe. Mzeru, ya kutoa mifuko hiyo 100 ya Saruji, ilitokana na ziara yake ya kikazi aliyoifanya Januari 17/2022 katika kutembelea madarasa mapya yaliyojengwa na fedha za Maendeleo na ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa