Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, mheshimiwa Pascal Kihanga, ametoa wito kwa waheshimiwa madiwani kuendelea kuwafariji wananchi wa baadhi ya Kata za Manispaa, zilizoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mavua nyingi zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Kihanga ameyasema hayo alipokuwa kwenye Kikao cha Kawaida cha Baraza la Waheshimiwa Madiwani cha Uwasilishaji wa Taarifa za Kata, kiolichofanyika jana, tarehe 23.01.2024, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro, ambapo pia amewataka waheshimiwa madiwani pamoja na watendaji wa Kata na Mitaa kuhakikisha wanaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu ambao kwa sasa upo katika baadhi ya mikoa nchini.
“Kipindupindu kimeshaingia kwenye mikoa mingine hivyo natoa rai kwenu waheshimiwa madiwani wenzangu tuendelee kuwapa wananchi wetu elimu ya kujikinga na ugonjwa huu, alisisitiza mheshimiwa Kihanga.
Kwa upande mwingine, katika kikao hicho waheshimiwa madiwani wa Kata za Kilakala, Bigwa na Kichangani waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata zao kwa kipindi cha Robo ya Pili ya Oktoba- Disemba, ambapo Diwani wa Viti Maalum Kata ya Kilakala, mheshimiwa Mwanaidi Ebrahim Ngulungu emesema kwenye Kata yake Serikali imefanikisha ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, mabweni manne na matundu 13 ya vyoo kwenye shule ya Sekondari Kilakala, pamoja na kuanza kwa upanuzi wa Zahanati ya Kata hiyo, huku wananchi wakiwa wamechangia jumla ya shilingi mia sita themanini elfu (680,000) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Kata yao.
Kisha Diwani wa Kata ya Kichangani, mheshimiwa Gilbert Barnabas Mtafani akasema, katika Robo hiyo ya Oktoba- Desemba, ndani ya Kata yake, Serikali imefanikisha ujenzi wa jengo la utawala kwenye shule ya Sekondari Kola Hill, na Diwani wa Kata ya Bigwa, mheshimiwa Melichior Peter Mwamnyanyi akasema kwenye Kata yake Manispaa, kupitia fedha za mapato yake ya ndani, imefanikisha ujenzi wa matundu sita ya vyoo kwenye shule ya msingi Mungi huku wananchi wakiwa wanaendelea kuchangia ujenzi wa matundu ishirini ya vyoo kwenye shule ya msingi Misongeni.
Aidha Diwani wa Kata ya Kichangani, mheshimiwa Mtafani ameomba kuimarishwa kwa hali ya ulinzi na usalama ndani ya Kata yake, Diwani wa Kata ya Bigwa, mheshimiwa Mwamnyanyi akaomba miundombinu ya barabara iimarishwe,na Diwani wa Viti Maalum, Kata ya Kilakala mheshimiwa Ngulungu, akasema changamoto inayokabili Kata yake ni uchakavu wa miundombinu na wananchi kutokamilisha miradi wanayoianzisha.
“Mvua zinazoendelea kunyesha zimeharibu miundombinu ya barabara hasa maeneo ya Area 6 na, Njiapanda ya Jordan. Zimeondoa sehemu iliyojengwa mto Kilakala, pia nyakati za jioni maeneo ya Kola A na B, hivi sasa kumekuwa na tabia ya ukwapuaji” alibainisha Diwani wa Kata ya Kichangani, mheshimiwa Mtafani.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa