MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 21/2022 katika Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Morogoro lililofanyika katika Ukumbi wa Savoy Morogoro Manispaa.
Akizungumza katika Jukwa hilo, Mhe. Kihanga, amesema kutofanya kazi kwa kuzingatia uadilifu kuna pelekea ubadhilifu wa fedha pamoja na migogoro ndani ya ushirika.
“Lazima mfanye kazi kwa uadilifu , msiruhusu migogoro,mkiwa na migogoro hata wale wanaotaka kutoa misaada hawatawaletea tena, simamieni miiko ya Uongozi ili Wanachama wenu waweze kunufaika na Ushirika huu” Amesema Kihanga.
Aidha, Kihanga, amewataka Viongozi kufanya kazi kwa kusimamia sheria na kanuni badala ya kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo halitawafikisha mbali na kutofika mafanikio au malengo waliojiwekea.
Hata hivyo, amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha katika Mikutano yao agenda kubwa iwe uadilifu ili kujenga uwaminifu kwa wanachama wao.
Kuhusu changamoto ya vyama vya mazao, amezitaka Taasisi za kifedha kuvitembelea vyama hivyo na kuweza kutatua changamoto zao.
Naye Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Idd Rajabu, amesema lengo la Mkutano huo wa Jukwaa la Vyama vya Ushirika ni kuwakutanisha wana Ushirika na wadau wake kwa ajili ya kujengeana uwezo na uzoefu ili kujenga Ushirika Imara na wenye nguvu.
Kwa upande wa Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Keneth Shemdoe, amesema kazi kubwa ya kufanya katika kuimarisha Vyama Vya Ushirika ni kutoa elimu na ushauri, usimamizi na ukaguzi .
Shemdoe ,amesema kuwa katika Mkoa wa Morogoro kuna jumla ya upungufu wa Maafisa Ushirika 22, hivyo kuna kila haja ya kuweza kupata wataalamu hao ili kuimarisha vyama hivyo kwa ngazi za Halmashauri.
Mwisho, Shemdoe, amesema kwa sasa jukumu kubwa la Jukwaa la Vyama Vya Ushirika ni kuimarisha Masoko na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa