MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wazazi wa Wanafunzi Manispaa ya Morogoro kuhakikisha wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wote wanawasili shuleni ili kuweza kupata elimu na kutimiza ndoto zao baada ya Serikali kuwatengenezea mazingira rafiki ya kusoma.
Kauli hiyo ameitoa, Januari 20/2022 wakati wa ukaguzi wa Madarasa mapya katika Shule ya Sekondari Kihonda, ambayo madarasa hayo ni miradi ya elimu iliyojengwa kutokana na fedha ambazo Serikali imezipata kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na athari za UVIKO-19 na kuzielekeza kuimarisha huduma za jamii.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mhe. Kihanga, amesema kuwa hakuna mzazi anayeruhusiwa kukaa na mtoto bila kupelekwa shule labda kama ana changamoto za kiafya zilizothibitishwa na wataalamu wa afya.
Sambamba na hilo Mhe.KIhanga, amempongeza namna ambavyo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ,Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Baraza la Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wote, na wananchi kwa kushirikiana bega kwa bega hatimaye kupelekea madarasa yote 86 kukamilika kwa wakati Pamoja na kuwepo changamoto za miundombinu zilizopelekea baadhi ya sehemu kuendesha shughuli za ujenzi kwa kususua.
"Nampongeza sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia fedha hizi, tumenufaika kwani tumeweza kujenga madarasa na kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi ya elimu kwenye shule zetu , naamini mazingira haya yatapunguza msongamano madarasani lakini kuongeza viwango vya ufaulu , rai yangu wanafunzi wasome kwa bidii na kulinda miundombinu" Amesema Mhe. Kihanga.
Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri zilizopata fedha za Ujenzi wa Madarasa ambapo wamepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1 na Milioni 720 kwa kukamilisha ujenzi wa Vyumba vya Madarasa 86.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa