MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kuzingatia maadili ya kazi katika utendaji wao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 15/2020 wakati akizindua mafunzo ya Maadili kwa Madiwani wa Manispaa hiyo ,yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Msamvu Kituo cha Mabasi.
Akizungumza na Madiwani , amesema semina hiyo ya mafunzo ya maadili ni somo muhimu kwa maisha ya kawaida na katika utendaji wao wa kazi katika kuwaongoza wananchi na kutoa huduma.
Amesema kiongozi asiyezingatia maadili kazini hata katika utendaji wake unakuwa na shida kutokana na kukosa misingi ya uadilifu ambayo ndiyo nguzo kuu ya utendaji kazi.
Mhe. Kihanga ,amesema miongoni mwa vitendo ambavyo vinasababisha kukosekana kwa uadilifu wa kazi ni pamoja na kupokea na kutoa rushwa, ubadilifu wa mali za umma, kuwa na mahusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi wenyewe, kutumia cheo kwa maslahi binafsi, mgongano wa maslahi, tabia ya ulevi , uasherati na ugomvi kwenye jamii ambapo vitu vyote hapo vinamuondolea sifa kiongozi kimaadili.
“Viongozi lazima tuwe waadilifu, hata Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Magufuli , amekuwa mfano kwa kujaza na kusaini hati ya uadilifu inayosimamiwa na tume ya maadili na viongozi wa Umma na viongozi wote tulioteuliwa tumekula kiapo hicho , kwahiyo tutambue kazi zote tunazo zifanya kwa wananachi wetu ni kwaniaba ya Mhe. Rais kwa kufuata maudhui na maadili kama Rais wetu anavyofanya, niwaombe sana mzingatie maadili lakini matarajio yangu ni kwamba Madiwani wote mtakula kiapo cha maadili leo “ Amesema Mhe. Kihanga.
Amesema kuwa matarajio yake baada ya mafunzo hayo madiwani watakuwa wameweza kupata maarifa ya kimkakati yatakayoweza kuwasaidia kuwaongoza Wananchi wao.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewaomba Madiwani kuwa wasikivu kwakuwa watoa mafunzo wamekuja kuwafundisha na wanajua nini ambacho wanatakiwa kuwasaidia .
Katika hatua nyingine, Lukuba, amewapongeza madiwani pamoja na Wakufunzi kwa kukubali kufanya semina hiyo huku akiwakumbusha na kuwaomba Madiwani kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili , kanuni na taratibu za nchi kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Nawashukuru sana wageni wetu kutoka tume ya Secretarieti ya maadili Kanda ya Mashariki Morogoro na Tanga , pamoja na Wakufunzi kutoka Chuo cha Hombolo Dodoma kwa kutukubalia kuendesha mafunzo yetu, naamini baada ya mafunzo haya tunategemea Madiwani wetu wataendesha kazi zao kwa kuzingatia maadili katika utoaji huduma kwa wananchi wao”” Amesema Lukuba.
Naye, Diwani wa Kata ya Kilakala, Marco Kanga, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa hatua mbalimbali za kuhakikisha Baraza la Madiwani linakuwa chachu ya maendeleo.
‘’Ni mafunzo mazuri upande wetu, hii sio mara ya kwanza lakini tunakumbushwa zaidi ili kuendana na mabadiliko ya uongozi uliopo madarakani ambapo uanataka kila kiongozi awe na maadili kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wake” Amesena Mhe. Kanga.
Kwa upande wa Afisa kutoka Secretarieti ya Maadili Kanda ya Mashariki Morogoro na Tanga , Zaynab Kissoky , amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutokana na changamoto mbalimbali katika upande wa maadili kwa Watumishi wa Umma kitu kinachopunguza ufanisi katika kufikia malengo ya kazi.
Mbali na mafunzo amesema Madiwani watajaza na kusaini hati ya uadilifu kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Umma.
Miongoni mwa maada zilizowasilishwa ni pamoja na Historia ya Uhalali wa Serikali za Mitaa, Sheria za Uendeshaji wa Mamlaka ya MSM, Muundo, Madaraka na Majukumu ya MSM,Maadili, pamoja na Taratibu za Uendeshaji wa Vikao na MSM.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa