Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa Morogoro Dkt. Maneno Fucus amefanya kikao na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wa kata za Manispaa na kuwataka wapeleke elimu ya afya ya mama na mtoto, magojwa yasiyo ambukiza, masuala ya lishe, ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto, dharula za kiafya, na usafi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Morogoro leo tarehe 22.03.2024 Dkt. Focus amewataka wahudumu hao kufahamu mifumo ya kutoa taarifa pindi dharula mbalimbali za kiafya zinapotokea kwenye maeneo yao waweze kuwasiliana na wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya wa Manispaa.
“Eneo la mama na mtoto bado tuko nyuma sana. Kwa mwaka 2023 tu tumekuwa na vifo takriban 200 vya watoto wachanga na akina mama 42 na bado tunapata wajawazito wanaofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wamechelewa sana yani bado dakika chache wajifungue kutokana na sababu mbambali ikiwemo imani potofu kwamba ukiwahi kwenda hospitali utafanyiwa upasuaji.
“Nendeni mkawahimize wanawake wawe wanaanza kliniki chini ya wiki 12 za ujauzito maana kuna vipimo muhimu hufanywa wakati huo ikiwemo kipimo cha wingi wa damu ili kama kuna upungufu uanze kushughulikiwa mapema ifikapo muda wa kujifungua mjamzito asipate shida, pia kupitia vipimo vya awali tunaweza kuzuia wajawazito wasipate watoto wenye changamoto za kimaumbile kwa sababu watapewa madini muhimu yanayosaidia uumbikaji wa mtoto” alifafanua Dkt. Focus.
Kwa upande wa elimu ya lishe, Dkt. Focus amewataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa wajawazito, wazazi, walezi wa watoto kwani vichanga wengi waliofariki mwaka jana 2023 vifo vyao vilisababishwa na uzito mdogo unaoweza kuchangiwa na lishe duni kwa mama wakati wa ujauzito.
Eneo lingine ambalo Dkt. Focus amelizungumzia ni la ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, ambapo amewataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii waibue matukio ya ukatili kwenye maeneo yao na kuyatolea taarifa kwa maafisa ustawi wa Manispaa waliopo kwenye kata na makao makuu kwa ujumla. Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuondoa ukatili huu ambao unaweza kumwachia madhara ya kudumu ya kisaikolojia mtoto aliyefanyiwa vitendo hivyo.
Aidha, Dkt. Focus amewataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoa elimu ya afya kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kama vile shiniko la damu na saratani mbalimbali ili wananchi wawahi kwenda kupima na kupewa matibabu na ushauri wa kiafya pindi wanapokuwa na dalili za magonjwa hayo, na kwa walioanza matibabu wahimizwe kuendelea kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata huduma zaidi.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto wa Manispaa ya Morogoro ndugu Vijan Shaban amesema, jambo kubwa analowataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii kulifanya kwenye maeneo yao ni kuifundisha jamii dalili za hatari za wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ili kuzuia vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.
Pia amewataka wahudumu hao kupeleka kwa jamii elimu ya uzazi wa mpango kwani inaonesha vifo vingine vya mama na mtoto vinasababishwa na akina mama kubeba ujauzito mfululizo bila kupumzika.
Nao wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamemshukuru sana Mganga Mkuu wa Manispaa pamoja na timu yake kwa kufanya nao vikao mara kwa mara kisha wakaahidi kwenda kutekeleza yale yote ambayo wameagizwa kuyafanya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa