Usiku wa Machi 17.2021 ulikuwa mzito sana na watanzania waligubikwa na majonzi baada ya kupokea taarifa ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliyekuwa Makamu wa Rais kwa wakati huo, ambaye hivi sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye alilihutubia Taifa akiwa amejaa majonzi hata alishindwa kuzuia macho yake kububujikwa machozi wakati alipokuwa akilieleza taifa habari za kifo cha Hayati Magufuli.
Hakika Tanzania ilizizima. Sio watoto, sio vijana, sio watu wazima, sio wazee, kila mtu kwa namna yake aliguswa na msiba huo na habari zikaenea kila pembe ya dunia, salamu za pole zikaanza kumiminika nchini huku taratibu zikiandaliwa kuhakikisha nchi inapata kiongozi wa kuishikilia na kuiendesha katika wakati huo wa majonzi.
Tarehe 19.03. 2021 ndipo aliyekuwa makamu wa Rais, mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikula kiapo cha kuiongoza nchi ya Tanzania kama Rais.
Sio ajabu kwamba maswali na mashaka miongoni mwa watanzania yalikuwa mengi kuhusu utawala wa Rais Dkt. Samia, huenda wengine walibeza ikiwa kweli ataweza kuiongoza nchi ya Tanzania ilhali yeye ni wa jinsi ya kike na haikuwahi kutokea hapo kabla nchi ya Tanzania kuwa na kiongozi mwanamke sio tu katika ngazi ya Makamu wa Rais bali hata ngazi ya urais yenyewe.
Mara tu baada ya kula kiapo cha urais, mheshimiwa Dkt. Samia alihutubia taifa na kuwatia moyo watanzania kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hicho kigumu cha majonzi na tangu hapo aliendelea kuongoza taratibu zote za msiba mpaka mwili wa Hayati Dkt. Magufuli ulipolazwa kaburini.
Siku moja Rais Dkt. Samia alihutubia taifa na kuwaondolea wasiwasi watanzania kwamba japokuwa yeye ni wa jinsi ya kike, ndiye Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wasiwe na mashaka naye katika kuendeleza gurudumu la urais nchini. Kisha akatambulisha salamu mpya nchini iliyobeba kauli mbiu yake akasema nikisema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, mtatakiwa kujibu “Kazi Iendelee”.
Hakika tunaiona kazi ikiendelea nchini kwani Rais Dkt. Samia tangu amekuwa madarakani miaka mitatu sasa, hajaacha kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo mtangulizi wake, Hayati Dkt. Magufuli aliianzisha ili kuifungua kiuchumi Tanzania, ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya mwendo kasi, ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa madaraja kama vile Tanzanite, na Wami, ujenzi wa barabara za lami, na bandari kavu.
Katika ngazi ya Serikali za Mitaa nako miradi ya afya, elimu, biashara na uchumi nayo imekuwa ikiendelea na sio kuendelea tu bali Rais Dkt. Samia amekuwa akielekeza pesa nyingi katika kuimarisha huduma muhimu ambazo Serikali imeazimu kuhakikisha zinawafikia wananchi kwa ubora na ufanisi.
Manispaa ya Morogoro inayo mambo mengi ya kujivunia ndani ya miaka mitatu ya utawala wa Rais Dkt. Samia katika ufikishaji wa huduma za afya, elimu, kilimo, biashara, maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, makazi na utawala kwa jamii. Mabilioni ya pesa yamekuwa yakiletwa na Serikali kuhakikisha shughuli zote za kisekta zinatekelezwa, na wananchi wa Manispaa ya Morogoro wananufaika.
Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni mojawapo ya shughuli kuu ambazo Halmashauri zote nchini inafanya, na Manispaa ya Morogoro katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala na uongozi wa Rais Dkt.Samia inayo ya kujivunia katika eneo hilo hasa kwa upande wa huduma za jamii kama vile elimu, na afya.
Katika sekta ya afya, vituo vya afya viwili vimejengwa, Hospitali ya Wilaya inajengwa na Zahanati 10 zimejengwa. Ujenzi huu unafanya utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi wa Manispaa kuwa imara na rahisi zaidi na kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa. Pia unaifanya Manispaa kuwa na jumla ya vituo vya afya 7 vya Serikali, Zahanati 27, na Hospitali moja.
Kwa upande wa sekta ya elimu msingi, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi na utawala wa Rais Dkt. Samia, Manispaa imejenga shule mpya za msingi tatu, matundu 63 ya vyoo kwenye shule mbalimbali, vyumba vya madarasa 143 kwenye shule mbalimbali, na ujenzi wa bweni moja lenye uzio kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu unaendelea kutekelezwa Kihonda.
Shughuli hizo zimepanua utoaji wa huduma ya elimu ya awali na msingi kwa Manispaa na inaifanya Manispaa kuwa na jumla ya shule za msingi 75 za Serikali zinazohudumia wanafunzi 69,071, wakiwemo wavulana 34,385 na wasichana 34,686, na kazi bado inaendelea, hakuna kilichosimama.
Elimu Sekondari nayo haijaachwa nyuma. Katika miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia, Manispaa imejenga shule mpya 7, vyumba vya madarasa 194, maabara za sayansi 11, majengo ya utawala 7, Ofisi ndogo za walimu 9, Nyumba za watumishi 4, mabweni 5, na matundu ya vyoo 56.
Ujenzi huu umeifanya Manispaa kuwa na shule za sekondari 30 kwenye kata zake 28 kati ya 29, na tafsiri yake ni kwamba sekta ya elimu sekondari inaendelea kuimarika.
Upande wa bishara na uchumi, Manispaa inajenga jengo kwa ajili ya wafanya biashara wadogo maarufu kama machinga. Mwaka huu jengo hilo linatazamiwa kukamilika na machinga zaidi ya mia mbili wataendesha biashara zao ndani yake.
Hii pia inaonesha Serikali inavyojali wafanyabiashara wa hali zote, wakubwa kwa wadogo na hii ndio tafsiri halisi ya kuwapelekea wananchi maendeleo na kuboresha hali zao za maisha.
Katika kuimarisha makazi kwa wananchi, Serikali kupitia sekta ya mipangomiji ya Manispaa ya Morogoro imehakiki, kupanga na kupima viwanja 11, 911 kwenye eneo la Kiegea A na B lenye ekari 4500 kwa gharama ya shilingi bilioni moja.
Wananchi zaidi ya elfu tatu waliokuwa na changamoto za migogoro ya ardhi wamefidiwa na wananchi wenye uhitaji wa viwanja vya makazi na biashara wamekuwa wakiuziwa viwanja kwa bei nafuu.
Wananchi wanaotoka kwenye kaya maskini nao wanaendelea kupatiwa msaada wa fedha pamoja na kujengewa uwezo wa kujiajiri kupitia mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wamekuwa wakipatiwa mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuibua miradi itakayowainua kiuchumi.
Ingawa wakulima wa Manispaa wanatekeleza kilimo cha mjini, Serikali iko pamoja nao na inawapatia huduma za ugani na mbolea za ruzuku, mradi ambao umeanzishwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya utawala na uongozi wa Rais Dkt. Samia nchini.
Watanzania hawana shaka na utawala na uongozi wa Rais Dkt. Samia kwani katika kipindi hiki cha miaka mitatu amedhihirisha umahiri wake katika kuijenga Tanzania yenye utulivu, amani, upendo, umoja, na mshikamano kupitia sera yake ya R4 ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), Ustahimivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Ujenzi Mpya (Rebuilding).
Hakika watanzania tunashuhudia kazi ikiendelea kwa ufanisi na weledi, na hata makundi ya watu wenye mahitaji maalum, wazee, vijana, wanawake, na watoto, yanathaminiwa na kupatiwa huduma bora kwa ustawi wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Morogoro ndugu Emmanuel Mkongo, anatoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeendelea kuimarisha na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa