Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ndugu Ally Machela amewataka ananchi wote wenye kero za ardhi wiki ijayo wafike kwenye Ofisi za ardhi za Manispaa hiyo zilizopo eneo la stendi ya Mafiga kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kero zao.
Ndugu Machela ametoa wito huo alipokuwa akijibu hoja za wananchi wa kata ya Mkundi kwenye mkutano wa kusikiliza na kujibu kero za wananchi uliofanywa tarehe 25.02.2025 na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, mheshimiwa Rebecca Nsemwa, kwenye mtaa wa Mgulu wa Ndege Mkundi.
“Wiki ijayo tutaanza kliniki ya ardhi itakayodumu kwa muda wa wiki moja. Kamishina wa ardhi na Registrar wa ardhi watakuwepo, hivyo ye yote mwenye matatizo ya hati, double allocation, na migogoro ya ardhi kati ya mtu na mtu aje atapatiwa majibu” alieleza Machela.
Katika hatua nyingine ndugu Machela amewataka wananchi walioathiriwa na mafuriko yaliyotokea tarehe25.01.2024 wawe na subira kuona Serikali itashughulikia vipi madhara yaliyowapata, kwa kuwa timu ya taifa ya maafa ilishakuja na kufanya tathmini ya athari ya mafuriko hayo ambayo yaliathiri nusu ya kata 29 za Manispaa kwa jumla ya nyumba 554 kuingiliwa na maji na nyumba 161 kubomolewa kabisa.
Amewataka wananchi ambao bado wanaishi kwenye maeneo ya mabondeni waendelee kuhama kwenye maeneo hayo ili wasipatwe na madhara yakiwemo magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wa elimu, Mkurugenzi Machela amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Ofisi yake imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu, na ununuzi wa pikipiki tatu kwa ajili ya walimu wa shule ya msingi Ujirani ili kuwapatia ahueni ya mazingra ya kazi walimu wa shule hiyo.
Pia ameahidi kuezeka maboma mawili ya vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu ya wananchi kwenye mtaa wa Kilongo B na kwamba mara baada ya kuezeka wataanzisha shule shikizi ili wananchi wa mtaa huo waweze kuwa na shule ya msingi kwa ajili ya watoto wao.
Awali kabla ya kujibu kero za wananchi, Mkurugenzi Machela alieleza miradi ya maendeleo ambayo Serikali inaitekeleza kwenye kata ya Mkundi ikiwemo ujenzi wa machinjio ya muda, eneo la mnada wa mifugo kwenye mtaa wa Mawasiliano, ujenzi wa nyumba ya Daktari kwenye Zahanati ya Mkundi, ambayo itakapokamilika, Zahanati hiyo itafunguliwa na kuanza kuhudumia wananchi.
Naye Diwani wa kata hiyo mheshimiwa Seif Chomoka amesema shida kubwa waliyonayo wananchi wa Mkundi ni maji safi na salama, barabara za uhakikazinazopitika wakati wote, na umeme.
“Zaidi ya mitaa mitano kati ya mitaa kumi inayounda kata yangu hii ya Mkundi haina huduma ya umeme mpaka sasa, na suala la kuletewa maji safi na salama limechukua muda mrefu sasa kukamilishwa, hivyo ninaomba mambo haya yashughulikiwe ili tuweze kudumisha uaminifu wa wananchi wetu kwa Serikali yao” alieleza Chomoka.
Kwa upande wao wananchi wamemshukuru sana Mkurugenzi wa Manispaa kwa kushirikiana vyema na Diwani wa kata yao kuhakikisha wanawaletea maendeleo katani humo ambapo wameeleza jinsi mheshimiwa Diwani wao alivyoanzisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Mlimani kwa kujenga vyumba vitatu vya madarasa na baadae Ofisi ya Mkurugenzi ikaongeza vyumba vingine 11 na kujenga jengo la utawala la kisasa kwa ajili ya walimu wa shule hiyo.
“Mwaka huu tumeshuhudia wanafunzi wa kidato cha pili wa shule yetu ya Mlimani wamepata ufaulu mzuri sana. Hii inachochewa na uwepo wa jengo la utawala na madarasa yanayofanya mazingira ya ufundishaji na ujiunzaji yawe mazuri zaidi” alieleza mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutanoni hapo.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa