MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewaonya Wakandarasi wazawa kuacha tabia ya kujikongoja wanapoaminiwa na kupewa miradi mikubwa katika Manispaa yake , huku akionyesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya Ujenzi wa Kitega Uchumi DDC unaoendelea kwa sasa.
Hayo ameyasema leo Mei 13,2020 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Lukuba ,amesema kuwa ni lazima wahakikishe miradi wanayokabidhiwa na Serikali inakamilika kwa wakati.
Kufuatia kudolora kwa ujenzi wa DDC, Lukuba, amemuagiza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng.Juma Gwisu, kuhakikisha muda waliopewa wa ujenzi wa mradi huo wakamilishe na hana mpango wa kuongeza muda mwengine.
“”Hawa ndugu zetu tuliwaamini sana , walianza kwa kasi kubwa licha ya kuwaongezea muda lakini bado sijaridhishwa na kiwango cha Ujenzi wa mradi huu,nimeongea na msimamizi wa mradi huu analeta sababu zisizo na msingi wakati tayari tumelipa fedha, najua waliomba waongezewe muda lakini hapana ni bora ningekuta kuna maendeleo ninge fikiria lakini bado hali ipo vile vile “ Amesema Lukuba.
Aidha, amemtaka msimamizi wa ujenzi huo kuongeza nguvu kazi ili ujenzi uendelee kwa kasi kwani muda uliobakia ni mdogo sana.
Lukuba, amesema kuwa, kwa mujibu wa mkataba ujenzi huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 635, ulitakiwa kukabidhiwa mwezi Mei 20,2020 lakini mpaka sasa haujakamilika licha ya kuongezewa muda wa mwezi 1 ambapo sasa watatakiwa kuukabidhi mwezi Mei 25, 2020.
Katika hatua nyengine, Lukuba, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Stendi mpya ya Daladala Mafiga huku akimtaka Mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi zaidi na kuukabidhi mradi huo kwa wakati kama walivyokubaliana.
“Nimefurahishwa na kasi ya ujenzi huu wa Stendi ya daladala , tumekubaliana mpaka ikifika Mei 25,2020 wawe wametukabidhi mradi huu , niwaombe waongeze kasi ili tukabidhi mradi huu kwa wananchi ambao wamekuwa wakiusubiria kwa hamu sana, endeleeni kufanya kazi usiku na mchana natumaini hiyo asilimia 4% iliyobakia mtaimaliza kwa wakati”” Amesema Lukuba.
Hata hivyo, amewaeleza wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa Serikali yao ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ipo makini na itahakikisha ina kamilisha kwa asilimia 100 miradi yote ya maendeleo ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mwisho, amewataka wakandarasi wote wanaosimamia miradi katika Manispaa ya Morogoro, wafanye kazi kulingana na walivyosainiana mikataba kwani fedha ambazo wanatumia ifikapo mwezi Juni 30, 2020 zitarudishwa hivyo kuna athari ya wenye miradi na waliochukua tenda kuzikosa fedha hizo.
Kwa upande wa Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu, amesema atahakikisha fedha za miradi hazirudi Serikalini , hivyo atakula nao sahani moja wakandarasi ili fedha hizo ziendelee kutumika katika miradi hiyo.
Gwisu , amesema ujenzi wa mradi wa Stendi ya Daladala Mafiga mpaka sasa umefikia asilimia 96% huku miradi mingine ikiendelea vizuri na ujenzi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa