MKURUGENZI wa Manipsaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, leo Novemba 20, 2019, amefungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara juu ya uzingatiaji wa kanuni, sheria na taratibu za Utumishi wa Umma.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho , amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Wakuu wa idara pamoja na kutoa huduma bora na kuzingatia miiko ya kazi na kuweka malengo halisi ya kazi ili kufikia kiwango cha juu katika utendaji wa kazi .
Amesema kuwa mafunzo hayo yameendeshwa na wawezeshaji kutoka Chuo kikuu Mzumbe , hivyo amewaomba watumishi kuzingatia mafunzo hayo muhimu kwani yanawajengea uwezo watumishi kimaadili katika kazi zao za kila siku.
"Tumewaandalia mafunzo haya ikiwa ni sehemu ya wajibu wangu kama mwajiri wenu wa kuwajengea uwezo ili hatimaye muweze kuongeza ufanisi wa kazi kila mmoja katika eneo lake la kazi, nyinyi ni watu muhimu sana kwenye taasisi yoyote, nawaomba mjiamini vya kutosha ,muwe familia moja." Amesema Sheilla.
Aidha, amekipongeza Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kujitoa kwao katika ushirikiano wa mafunzo hayo pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, akisema matarajio yake ni kwamba baada ya mafunzo hayo watumishi watazingatia vizuri miiko ya kazi na kutoa huduma bora kwa Wananchi pamoja na kutunza siri za ofisi.
Naye Afisa Utumishi wa Manispaa ya Morogoro Waziri Kombo, amesema mafunzo hayo yamehudhuriwa na jumla ya Wakuu wa idara 19 na wasaidizi 30, huku akitarajia kila mkuu wa idara na wasaidizi wake mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo watatoa huduma bora kwa Wananchi wao.
Pia amesema kuwa,mafunzo hayo yamewalenga wao kwani ndio wanaosimamia idara hivyo amewataka wabadilike na kuendana na kasi ya Mhe.Rais Dkt John Magufuli ya kuchapa kazi kwa bidii pamoja na kufuata misingi ya utawala bora.
" Niwaombe watumishi wenzangu, ufanyaji kazi umebadilika, Rais wetu anahitaji matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa, hivyo lazima tubadilike ili kuendana na kasi yake pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa muda wa kusikiliza Wananchi na muda wa kufanya kazi zako"" Amesema Kombo
Katika hatua nyengine, Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Morogoro, Ndg. Mohamed Chamzhim, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatawajengea uwezo mkubwa wa kuwatumikia wananchi na kutoa huduma bora ikiwamo kuzingatia miiko kazini na kuweka malengo ya kiutendaji.
Kwa upande wa Mratibu wa Kuzuia na kudhibiti maambukizi ya Ukimwi, Manispaa ya Morogoro, Upendo Elias, amesema wao wameyapokea mafunzo hayo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wakufunzi wa mafunzo kwani yataleta tija kubwa katika utoaji wa huduma bora.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa