MKURUGENZI wa Halmashauri ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amemtaka Afisa Mazingira na usafishaji Manispaa ya Morogoro kuhakikisha anaweka mikakati ya kueleweka katika uendeshaji wa dampo la takataka lililopo kata ya Mafisa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari , amesema hajaridhishwa na Uongozi wa Dampo hilo kutokana na uharibifu unaoendelea kufanywa na Viongozi hususani katika suala zima la uchimbaji wa Vifusi vya mchanga na kuvipeleka sehemu isiyojulikana.
Aidha, amesema katika kikao cha kusikiliza na kutatua kero za Wananchi mnamo Januari 8, 2020 kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi, St. Monica Kihonda, kuliibuka kero za kwamba kuna zoezi la uchimbaji wa Vifusi unaoendelea katika Dampo hilo.
"Nipo hapa Dampo, ni kweli nimejionea mwenyewe uharibifu uliopo kiasi kwamba taka taka zinashindwa kufikishwa sehemu husika kwa jinsi dampo lilivyoharibika, viongozi wa dampo hili wanahusika moja kwa moja kwani badala ya kutoa maelekezo ya umwagaji mzuri wa taka wao wanaruhusu taka kumwagwa njiani, nimemwagiza bwana afya hili swala alishughulikie na wale wote waliohusika nitawachukulia hatua " Amesema Sheilla.
Amesema kilichomsikitisha zaidi ni kwamba mtambo wa gari wanalozolea kifusi ni wa Manispaa na mafuta wanatoa Manispaa lakini hakuna hata pesa au chanzo chochote cha mapato wanachokipata kutoka katika dampo hilo jambo ambalo hawezi kulivumilia huku akimtaka bwana afya kuwa mkali la sivyo wote watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na matumizi mabaya ya mali za Umma.
Katika hatua nyengine amesema kama bwana afya hata kuwa mkali kwa hilo na kushindwa kuchukua hatua atatafuta mwenyewe walinzi watakao kuwa wanalinda na kuweka Uongozi utakaokuwa na maslahi kwa Manispaa na kuchangia mapato kwa ajili ya maendeleo.
Naye Afisa Mazingira na usafishaji Manispaa ya Morogoro, Samwel Subi, amesema wamepokea ushauri wa Mkurugenzi wa kusimamisha shughuli zote za uchimbaji Vifusi.
Pia amesema kuwa, kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za kuharibikiwa na mitambo miwili ya magari ya taka ambapo baada ya Mkurugenzi kutoa maelekezo wameshaanza kuyatengeneza na wana amini baada ya ya matengenezo hayo kero za taka zitakuwa zimetaturiwa na kuwaondolea wananchi kero ya moshi, harufu mbaya pamoja na kuzaliana kwa nzi.
Amesema kwa Sasa Manispaa ipo katika mchakato wa kutengeneza Dampo la Kisasa baada ya kupata eneo jipya Mkundi na kwasasa wapo katika mpango wa kulipa fidia kwani Dampo hilo kwa sasa lipo karibu na makazi ya watu hivyo kusababisha kero kwa wananchi.
Kuhusu uchimbaji wa Vifusi katika dampo hilo,amesema wameshatoa maelekezo kwa Meneja wa Dampo kwamba yeyote atakayeonekana anachimba kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Tumeshaongea na wananchi, Uongozi wa Mtaa pamoja na Mhe. Diwani wa kata hii ya Mafisa kwamba kama wataona mtu yeyote anachimba vifusi watoe taarifa kwa ajili ya utekelezaji wa kumchukulia hatua za kisheria, na kama ni mtumishi hatua za kinidhamu zitachukuliwa" Amesema Subi
Amesema kuwa Vifusi vilivyopo vitumike katika kufukia takataka katika dampo hilo, ili ziweze kuoza kwa urahisi na kuzuia nzi wasiendelee kuzaliana.
Kwa upande wa Mkazi wa eneo hilo, Yusuph Abdallah amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa hatua aliyochukua ya kupiga marufuku uchimbaji wa vifusi pamoja na kufuatilia maendeleo ya dampo hilo.
Amesema Uongozi wa Dampo hauwatendei haki kabisa kwani taka zimezagaa hovyo kiasi kwamba zinapelekea magonjwa ya milipuko.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa