MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewapongeza Wazazi wanaowasomesha watoto wao shule ya Msingi Mkundi kwa kujitoa na kusaidia ujenzi katika shule hiyo.
Akizungumza leo Januari 6, 2020 mara baada ya kutembelea shule hiyo kwa ajili ya kuangalia mwitiko wa wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2020, kufuatia mpango wa elimu bure bila malipo.
Amesema kuwa, kitendo cha Wazazi hao kuchangia kila mmoja Shilingi elfu 15 na tofali 3 ni makubaliano yaliyofanyika katika vikao na yakaandikiwa mihtasari kwaajili ya kupata kibali cha michango na hii ni baada ya Wazazi hao kuona wingi wa wanafunzi na changamoto ya madarasa, hivyo amekitaka kitendo hicho kiwe mfano wa kuigwa kwa wazazi wengine ikiwa ni mapokeo mazuri ya wazazi kutambua umuhimu wa kusaidiana na Serikali kwa Maendeleo ya Watoto wao.
"Hii ni hatua nzuri sana, na imeondoa ile dhana ya Wazazi kuachia Serikali peke yake baada ya kuona elimu inatolewa bure, ndugu zangu kuchangia sio dhambi, Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, amekuja na mpango wa elimu bure lakini sio kwamba kila kitu uiachie Serikali kwani elimu ina pembe tatu Mwanafunzi, Mwalimu pamoja na Mzazi, tukiwa kitu kimoja naamini hata matokeo ya ufaulu wa watoto wetu utaongezeka na kutengeneza Taifa lenye kuleta matokeo chanya hususani katika kuelekea uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda" Amesema Sheilla.
Aidha ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt John Magufuli kwa kubuni na kutekeleza mpango wa elimu bure bila malipo, jambo ambalo limesaidia sana wazazi kuwaandikisha watoto wengi tofauti na kipindi cha nyuma na asilimia kubwa ya wanafunzi imeongezeka katika uandikishwaji.
Kwa upande wao, Wazazi nao walichukua nafasi ya Kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Magufuli huku wakisema elimu bure imewasaidia na sasa hivi watoto wengi wameandikishwa na wanasoma lakini wameomba kuangaliwa kwa jicho la tatu na kusaidiwa pale watakapo ishia katika jitihada zao za kutatua changamoto shuleni.
Naye Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Abdul Buhetty, amempongeza Mkurugenzi kwa kutembelea shule hiyo lakini amemuomba kutatua changamoto zilizopo katika shule za msingi ili kuongeza viwango vya ufaulu na kuing'arisha Manispaa katika mitihani Kitaifa.
Amesema Shule ya Msingi Mkundi, kabla ya uandikishwaji wa wanafunzi wapya ilikuwa na jumla ya wanafunzi 2042 na sasa bado zoezi la uandikishwaji unaendelea.
Mbali na kutembelea Shule ya Msingi Mkundi pia ametembelea Shule ya Sekondari Kihonda Maghorofani.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa