MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amevigawia jumla ya Vituo 7 vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika Mazingira magumu pamoja na Wazee wasiojiweza ndoo za kunawia , sabuni pamoja na mabeseni ya kukingia maji machafu kwa ajili ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Akizungumza na kukabidhi ndoo hizo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Sidina Mathias, amesema ndoo hizo alizo zitoa Mkurugenzi ni moja ya jitihada za kuunga Mkono Serikali kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa CORONA .
Amesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa Makazi hayo ya Watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na Wazee wasio jiweza , Mkurugenzi ameona ni bora kuwapelekea ndoo ili zile pesa wanazopata ziweze kuwasaidia katika matumizi ya huduma nyengine.
“Leo tunatoa ndoo hizi kwa Makazi ya kulelea Watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na Wazee wasiojiweza, Mkurugenzi wetu kwa kutambua makundi haya yaliyopo katika Manispaa yake, ameona ni vyema akayakumbuka kwa kuyapatia ndoo za kunawia mikono, mabeseni pamoja na sabuni za kunawia katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya CORONA, amekuwa akishirikiana vyema na makundi haya katika kutoa misaada mbalimbali pamoja na huduma lakini hili alilolifanya leo ni jambo jema katika kuhakikisha wananchi hawa wanakuwa salama dhidi ya Ugonjwa huu”Amesema Sidina.
Kwa upande wa Mfawidhi wa Makazi ya Wazee wasiojiweza Funga funga, Bi.Rehema Kombe, amemshukuru sana Mkurugenzi wa Manispaa kwa jitihada zake za kuwajali Wazee hao.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi wetu, ameonyesha ni jinsi gani anavyojali afya za Wananchi wake, nakumbuka hii sio mara ya kwanza kutusaidia katika Makao yetu , alishawahi kutupatia TV pamoja na King’amuzi kwa gharama zake na upendo wake, kikubwa tunazidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ambariki kwa kile alichokitoa hakika tumepata Mama anaye tujali, kwa kutambua mchango wake pongezi hizi hazitaishia kwa maneno pekee bali tutamwandikia barua ya shukrani kwa jinsi anavyozidi kujitoa na kuonyesha upendo kwetu na kuwatia faraja Wazee hawa”Amesema Kombe.
Naye, Mlezi wa kituo cha kulea watoto Mgolole, Sister Palagia Maria , amesema alichokionyesha Mkurugenzi ni upendo kwa Watoto na kuwajali katika afya zao dhdi ya mapambano ya Virusi vya CORONA.
“Mkurugenzi wetu amekuwa akijitoa sana, hivi karibuni akiambatana na Mkuu wa Wilaya wa Morogoro Mhe. Regina Chonjo , walishawahi kuja hapa wakatupatia msaada wa Vyakula ,hivyo huu ni mwendelezo wa kutuunga mkono na tunamuomba aendelee kututhamini na kutusaidia asichoke yeye ni Mama yetu tunapokwama anatakiwa atukwamue, hiki sio kidogo amejinyima na familia yake na kuja kutuletea hapa tunampongeza sana na kumtakia majukumu mema ya kazi zake na kuifanya Manispaa yetu kupiga hatua zaidi za Maendeleo”” Amesema Sister Parakia.
Naye Mwenyekiti wa Wazee hao, Mzee Joseph Kaniki, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwajali na kuwathamini katika kipindi hiki cha mapambano ya Virusi vya CORONA.
Katika hatua nyengine, Sidina, amesema huu ni mwanzo , hivyo Mkurugenzi amejipanga na timu yake ya Wataalamu wa Afya kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Morogoro, chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Regina Chonjo kuhakikisha elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya CORONA inatolewa kila kona katika kulinda hali za afya za Wananchi wao.
Miongoni mwa Makao yaliyopatiwa ndoo, sabuni na mabaseni ni pamoja na Makao ya kulelea Watoto Mgolole, Makao ya kulelea Wazee wasiojiweza Funga funga, Raya, Agape Children’s Village, Dar-Ul- Muslimeen , Mission To The Homeless Children.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa