MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameitaka jamii ya Manispaa ya Morogoro kushiriki kwa vitendo katika ujenzi wa miundo mbinu ya elimu ili jamii iondokane na ujinga na kupata mafanikio ya haraka .
Kauli hiyo, ameitoa leo Julai 08,2020 , wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Madarasa 2 pamoja na Jengo la Ofisi ya waalimu katika Shule ya Sekondari SUA Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Lukuba, amesema ziara ya leo ni kukagua na kuangalia maendeleo ya Ujenzi wa Madarasa 2 na Jengo la Utawala ambapo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Sanare, alitoa maagizo juu ya Ujenzi huo baada ya vuta ni kuvute baina ya Kata mbili kufuatia kile kilichodaiwa ni mgogoro wa kimipaka.
Lukuba, katika ziara hiyo amewasisitizia mafundi kwenda na kasi kubwa ili wanafunzi waanze kuyatumia madarasa hayo katika kupunguza msongamano darasani.
‘’ifike wakati sisi jamii ndio tuwe wa kwanza kuanzisha miradi kisha ndio serikali iwekeze nguvu zake, nimekuja kuona maagizo ya Mkuu wa Mkoa yanatekelezwaje, lakini na mwagiza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro aongeze kasi ya kuwasismamia mafundi, wanafunzi wetu wana uhaba wa madarasa hatutaki mrundikano, tunataka yakamilike wanfunzi wasome katika mazingira ya kuachiana nafasi na Waalimu wetu wakae katika Ofisi nzuri na rafiki ili kuongeza kasi ya ufaulu, ukiwa katika mazingira mabaya hata ile hali ya ufundishaji inashuka, kazi nimeiona inaendelea lakini ongezeni kasi tumalize kazi mapema" Amesema Lukuba.
Lukuba, amesema kuwa Jamii inaposhiriki ipasavyo kwa vitendo katika ujenzi wa miundo mbinu ya elimu huwa chachu ya kupata kilicho bora kabisa maana jamii huwa na uchungu nacho kutokana kuwekeza nguvu zao na huwa walinzi wakubwa.
‘’Nawagiza watendaji wa vijiji na kata kwa wale wote watakao taka kujitolea katika ujenzi huu wa taifa katika vijiji na kata ambapo miradi hiyo inafanyika fuateni sheria ndogo za vijiji zilizotungwa katika jamii zetu kwa weledi kabisa ili kufikia malengo ya mradi kwa jamii kushiriki sawa’’ Ameongeza Lukuba.
Mwisho ametoa wito kwa wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro kuwa tayari kujitolea kwa hiari katika miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa