MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka viongozi na watendaji wa Manispaa ya Morogoro kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,na kuwaasa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kutimiza wajibu wao wa kufanya kazi.
Sheilla, ameyasema hayo Januari 8, 2020 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi St. Monica, alipokutana na Wananchi wa Kata tano ikiwemo Kata ya Lukobe, Mafisa, Kihonda, Kihonda Maghorofani pamoja na Mkundi katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amewataka watendaji kata, Mitaa, Wenyeviti wa Mitaa , Madiwani na wakuu wa Idara zote katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Amesema lengo la Ziara hiyo ni kutatua kero zinazowakabili wananchi, huku akisema kuwa mlundikano wa kero zilizopo mtaani zinatokana na kutowajibika kwa Watendaji wa ngazi ya chini.
Amesema hataki kuona tena Kero hazitatuliwi katika ngazi za chini ambapo zinaweza kusikilizwa na Mtendaji wa mtaa, Mwenyekiti wa mtaa, Mtendaji kata,au Afisa Tarafa.
" Viongozi nawaomba mtatue hizo kero ili kuendana na Kasi ya Mhe.Rais Magufuli ya kufanya kazi kwani hapa kazi tu na kuweza kuendana na Ilani ya Chama inatutaka tufanye kazi za kuwasikiliza Wananchi " Amesema Sheilla.
Katika Ziara hiyo amesema zipo Kero zilizopata ufumbuzi papo kwa papo na nyingine zilizochukuliwa na kupelekwa katika ngazi husika ambapo ni katika hatua mbalimbali za kutafutia Ufumbuzi.
Aidha katika Mgogoro wa Afya amataka wauguzi Pamoja na wafanyakazi katika sekta ya Afya wanaotumia lugha mbaya na chafu kwa wagonjwa kuacha tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesisitiza kuwa viongozi watakaoona kwamba hawawezi kuendana na kasi hiyo, kwa kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zao pamoja na kutotimiza majukumu yao ipasavyo, wajitoe wakafanye kazi nyingine kabla ya kusimamishwa kazi huku akieleza kuwa wananchi wengi hawasikilizwi kero zao na kwamba kero kubwa waliyokutana nayo ni migogoro ya ardhi.
Alifafanua kuwa viongozi wa mitaa na Kata wamekuwa chanzo cha migogoro hiyo kwa kuwasaidia wavamizi kuchukua maeneo ya wananchi ambapo wamekuwa wakiwagongea mihuli ilihali wanafahamu kuwa sio maeneo yao.
Amesema lengo la Serikali za mitaa ni kusogeza huduma karibu na wananchi na Kila kiongozi katika ngazi mbalimbali aliyechaguliwa, kuteuliwa au kuajiriwa anapaswa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Aidha amesema wamejipanga kuhakikisha kuwa wanaongeza mapato ya ndani kupitia Vyanzo vipya vya mapato, ikiwamo Miradi ya Kimkakati kama vile Soko Kuu la Kisasa , Stendi ya Mabasi Msamvu, Stendi mpya ya Daladala Mafiga na stendi ya daladala Kaloleni.
Katika hatua nyingine amewataka watendaji wa Kata na Mitaa kufanya vikao angalau Mara moja kwa mwezi ili yeye akiwa katika ziara zake akutane na Kero za maendeleo tu na zile ndogo ziwe zimetatuliwa na Watendaji hao.
Kuhusu kutokukamilika kwa baadhi ya miradi, amesema wale wakandarasi waliopewa Pesa za Serikali na Manispaa kama hawajamaliza miradi kwa wakati watamalizia kwa Pesa zao na kuwataka kukamilisha kwa wakati ili kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Mafisa , Mhe. Daud Salum Mnadi, amemuomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, kuwasaidia katika kukamilisha Kituo cha Afya cha SINA, ujenzi wa Soko la kata ya Mafisa , na kukarabati barabara za kata hiyo.
"Mkurugenzi Kituo chetu cha afya kilikuwa kinatoa huduma za Mama na Mtoto lakini baada ya kukatiwa maji hadi leo huduma hizo zimekata, tunakuomba utusaidie ili huduma hizi ziendelee kupatikana hapa, ukiangalia upande wa barabara hazipitiki hivyo kwa kikao hiki kilichotukuka naimani haya tuliyokueleza mbele ya hadhara utayafanyia kazi na kutatua changamoto zetu ili wananchi hawa waone jinsi tunavyopambana na matatizo yao nakuendelea kutuamini tena kuwaongoza katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka huu 2020" Amesema Mhe. Mnadi.
Pia Mkurugenzi amewaagiza Afisa Mazingira pamoja na TARURA wasimamishe haraka zoezi la uchimbaji wa Kifusi kilichopo Dampo la Kata ya Mafisa hadi pale watakapomletea kibali kilichowaruhusu kuchimba kifusi katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, amesema tatizo la kuchelewa uzoaji wa taka taka , linatokana na uzembe wa wakandarasi waliochukua tenda na kuwa na uwezo mdogo na kutokufanya kazi kwa usahihi na kuahidi kubadilisha mfumo wa kuwaondoa na kutangaza tenda mpya kwa makampuni yenye uwezo wa kufanya kazi.
Mstahiki meya wa Manispa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amempongeza Mkurugenzi kwa kushirikiana na timu ya Wataalamu wake wakuu wa idara pamoja na wakuu wa Taasisi za Serikali kwa kuwafuata wananchi jambo ambalo linawafanya Wananchi waweze kuwa na imani na kuwaaminisha kwamba Serikali yao ni Serikali ya kazi kweli.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa