Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro kutumia fursa ya mikopo kujiendeleza kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 12/2021 ikiwa ni siku moja kupita tangia kufanyika kwa Mkutano wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 akiwa katika ziara aliyoambatana na Wakuu wa Idara wa Manispaa ya Morogoro ya kukagua baadhi ya vikundi vya vilivyokopeshwa mikopo ya asilimia 10.
Akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa Manispaa ya Morogoro inaendelea kuwawezesha wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ili kuweza kujiinua kiuchumi na itawasimamia katika kuhakikisha kuwa mikopo hiyo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inawanufaisha Wananchi.
" Naahidi kuendelea kuwaendeleza wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kuwashika mikono kwa kutoa mikopo ya asilimia kumi katika mapato ya ndani, kupitia idara ya maendeleo ya jamii nitaendelea kuwainua wananchi wa Manispaa ya Morogoro , lakini niwaombe hizo fedha mnazokopeshwa ziwe katika mzunguko na zirudishwe kwa wakati ili wengine wapate" Amesema Lukuba.
Aidha Lukuba, amesema kuwa , mikopo hiyo sio zawadi inayotolewa kwao bali wanatakiwa kurejesha kwa wakati ili kuongeza wigo wa utoaji mkopo kwa vikundi vingine vingi zaidi na kukuza uchumi wa wananchi kwa vikundi na mtu mmoja mmoja.
Katika hatua nyingine, Lukuba, amesema kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 Manispaa ya Morogoro imetenga kiasi cha zaidi ya Tshs.963,000,000.00 kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu. .
Katika ziara ya leo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Wakuu wa idara wametembelea madarasa 4 yaliyojengwa na TASAF kwa kila shule kwa shule mbili za Sekondari ikiwamo Shule ya Sekondari SUA na Mafiga pamoja na kuangalia ujenzi wa Shule Sekondari SUA .
Lakini pia ukaguzi wa Kikundi kazi cha ndani kilichopata tenda ya uzoaji wa takataka kupitia mkopo wa Manispaa cha M2 Smart , Kikundi cha ujasiriamali wa kushona Masweta cha Kasi Mpya na Silc Kata ya Kihonda, Duka la huduma za kifedha na bidhaa za vyakula la watu wenye ulemavu lililopo Stendi ya Mabasi Msamvu ikiwa na lengo la kuona maendeleo ya vikundi hivyo na kuona kama fedha walizopewa zimetumika kwa malengo yaliyotarajiwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa