Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ndugu Ally Machela, ameagiza wananchi wote wenye biashara za kupika na kuuza chakula, waliko kwenye maeneo hatarishi wafunge biashara hizo mara moja ili kuendelea kuwakinga wananchi dhidhi ya ugonjwa wa kipindupindu ambao athari zake zimeanza kuonekana kwenye baadhi ya maeneo ya Manispaa hiyo ikiwemo kata ya Mafisa.
Ndugu Machela ametoa agizo hilo alipokuwa akijibu hoja za wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, wa kusikiliza na kujibu kero za wananchi uliofanyika kwenye mtaa wa Mambi kata ya Mafisa, tarehe 14.02.2024, ambapo amesema mpaka sasa wagonjwa zaidi ya 20 wenye kipindupindu kutoka kata ya Mafisa wanaendelea kupewa matibabu kwenye kitup cha afya cha Mazimbu huku wengine hali zao ziliimarika na wakaruhusiwa kurudi kwenye makazi yao.
“Hatuwezi kuacha wananchi wetu wafe kwa kisingizio cha maisha magumu. Hatuwezi kukubali mtu aendelee na biashara ya kupika na kuuza chakula kwenye maeneo yasiyo sahihi halafu wananchi wetu wakadhurika. Tutaendelea kupita kila siku na kufunga maeneo yote ambayo biashara hizo zinafanyika, mpaka ugonjwa huu upite” alisisitiza Machela.
“Eneo hili ndio ambalo mpaka sasa bado hatujafanikiwa kulidhibiti dhidi ya ugonjwa huu. Ndio maana hadi leo bado mnawaona maafisa afya wetu wanazunguka kwenye mitaa yenu wakitoa vidonge vya kutakasa maji, wakitibu vyanzo vya maji na kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu” aliongeza kusema.
Mkurugenzi Machela pia alizungumzia suala la mto Morogoro kuhama na kusababisha maji yake kuathiri sana wananchi wa kata hiyo ya Mafisa ambapo amewataka wananchi waendelee kuwa na subira kwani hivi karibuni wataalamu wa bonde la mto ruvu watapita kwenye maeneo yote na kuweka alama mahali pote ambapo mto huo umechepuka ili waweze kuurudisha katika njia yake.
Vilevile, ndugu Machela amewataka wananchi wa Mafisa wafahamu kwamba uwepo wa dampo la taka ngumu na dampo la maji taka ndani ya kata hiyo ni kwa mujibu wa mipangomiji, hata hivyo kutokana na mji kukua na idadi ya watu kuongezeka na madampo hayo kuanza kuonekana kuwa ni kero kwa wananchi, Manispaa inajipanga kuhakikisha taka ngumu hazitupwi kienyeji kwenye dampo la taka ngumu na kwa upande wa dampo la maji taka, MORUWASA nao wamepata eneo kubwa zaidi huko Kiegea kwa ajili ya kumwaga maji taka. Hivyo taratibu zitakapokamilika dampo la maji taka litaelekezewa huko.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa