MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amefurahishwa na matokeo ya utendaji wa kamati ya Ushauri Wilaya na kuwataka wajumbe waendelee kuhamasisha jamii kwa ajili ya kuchangia masuala mbali mbali ya maendeleo katika Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema lengo la Kamati ya ushauri Wilaya ni kuhakikisha Manispaa inasonga mbele, hivyo wajumbe wasichoke na wawe huru kutoa mapendekezo yao kwa kuchangia mambo mbali mbali kwa mustakabadhi wa maendeleo ya Wilaya.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu , amesema wanafunzi waliofaulu darasa la saba mwaka jana 2018, wote walifanikiwa kujiunga na kidato cha kwanza, akisema hayo ni maendeleo ya jitihada za Wajumbe wa Kamati ya ushauri katika kukuza elimu kwa Manispaa ya Morogoro.
Aidha, amesema mwaka huu, Wanafunzi wote wa darasa la saba wamefaulu na wanatakiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2020, lakini kuna changamoto ya upungufu wa madarasa 35 na mpango uliopo ni kila shule ya Sekondari kuongeza madarasa mawili.
"Niwaombe Wajumbe wa kikao cha Kamati ya ushauri wilaya, endeleeni kuhamasisha jamii kwa ajili ya kuchangia ili tuweze kupata msaada wa ujenzi wa madarasa, maana wakisema wachukue idadi ya Wanafunzi 45 kwa kila darasa wengi wataachwa na watashindwa kufika kidato cha nne na kutotimiza ndoto zao" Amesema DC Chonjo.
Kuhusu Vijana wanaoosha magari nje ya Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi CCM, amesema alishatoa maagizo lakini nashangaa mpaka leo Vijana hao wapo na wanaendelea kuosha magari katika eneo hilo ambalo sio maalumu kwa kazi hiyo na agizo lake limepuuzwa.
" Afisa Mazingira hapa umenikosea, inaonesha umepuuza agizo la kamati, kazi nakupa wewe na wewe unakazi ya kusema agizo ni la DC basi kama huiwezi hiyo kazi niifanye mwenyewe kuwaweka mgambo na kazi haifanyiki ni kupuuza agizo langu, narudia tena hao vijana watoke na muwatafutie maeneo maalumu ya kuoshea magari, maeneo yetu mengi yana water table (mzunguko wa maji).Aliongeza DC Chonjo
Aidha, amesema suala la mazingira kwa Manispaa ya Morogoro bado ni kizungumkuti, hivyo amemtaka Mstahiki Meya wa Manispaa na Mkurugenzi kupitia upya mikataba ya vikundi kazi vya usafishaji mji.
"Mhe. Mstahiki Meya nikuombe kaeni na baraza lako , suala la usafi Manispaa yetu bado ni tatizo, vikundi hivi havina uwezo wa kufanya kazi na watu wanalipa pesa zao taka hazizolewi kwa wakati kaeni mpitie mikataba yao upya na muone jinsi gani mnaweza kutatua changamoto hiyo kwani ni aibu Manispaa za wenzetu zinaongoza kwa usafi yetu hata kumi bora haipo " Amesema DC Chonjo.
Pia amemtaka Afisa Mazingira pamoja na MORUWASA kulifanyia ukarabati wa kuliziba shimo lililo pembezoni mwa Soko kuu kwani shimo hilo limekuwa kubwa kutokana na usugu wa kumwaga maji taka kwa wafanyabiashara wa mama lishe waliopo pembezoni mwa bara bara na kuleta athari kwa watumiaji wa bara bara hiyo.
Mbali na mazingira, DC Chonjo, amemuagiza Afisa biashara kuwaondoa haraka watu wanaodaiwa kufanya kazi mkabala na Soko kuu la kisasa kwani eneo hilo sio rasmi la wao kufanya biashara zao.
Akichangia suala la uharibifu wa bara bara , Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Ndg. Fikiri Hassan Juma, amesema kuna tabia imezuka ya malori makubwa kufanya maegesho ya magari pembezoni mwa barabara katika pande zote mbili jambo ambalo linahatarisha maisha ya watumiaji wa bara bara na kuharibu barabara kutokana na uzito wa malori hayo.
Akijibu hoja ya Maegesho, Meneja wa TARURA Mhandis James Mnene amekili kuwepo kwa changamoto hizo, lakini amesema wana kikosi kazi kinachotembea hadi usiku kwa ajili ya kuangalia maegesho ya malori makubwa barabarani.
Aidha, Mhandisi Mnene amesema kuwa tayari wale wahusika waliokamatwa tayari wamefikishwa mahakamani na kesi zipo kwa mwanasheria wao , huku akisema kuwa ushauri wa DC ameupokea na wataongeza jitihada zaidi ya kuyafanyia kazi mapendekezo ya Wajumbe wa kamati ya Ushauri Wilaya.
Kuhusu Ujenzi wa Darasa la Shule ya Msingi Tubuyu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Tubuyu, Justine Masaba, amesema darasa limeshatengenezwa na wapo katika hatua ya kutengeneza choo cha shule lakini Mkuu wa Wilaya amesema wale wote walisababisha hasara ya kujenga darasa jengine watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Morogoro aliyestaafu , Mhe. Steven Mashishanga, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kusimamia vyema mapendekezo ya kamati ya ushauri lakini amesema ni vyema katika vikao vijavyo vya kamati kila idara ikaonesha takwimu halisi katika taarifa zake zikiwamo changamoto , idadi ya upungufu wa watumishi ili kamati iweze kutoa ushauri.
Katika kuhitimisha hilo, DC Chonjo, amewataka Wananchi watakapoona kuna kero ambazo zinaleta madhara watoe taarifa kwake haraka ili kuzuia madhara yasiendelee kutokea.
Askofu Yohana, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kutokana na jitihada za kutokomeza vibaka na kuweka miundombinu mizuri ya barabara na kuwataka waendelee na kasi zaidi ili Manispaa iwe na maendeleo makubwa.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro, Ndg. Fikiri Juma, ameshauri kuwepo na usafiri kwa watumishi kwani kukosekana kwa usafiri kunawafanya watumishi kutofika maeneo ya wananchi kwa aharaka na kutoa huduma.
Aidha, amesema huduma ya zima moto kwenye nyumba za ibada ni changamoto, hivyo ameshauri MORUWASA na Zima Moto watenge maeneo ya kuchukulia maji inapotokea majanga ya moto.
Amesema bara bara ni nzuri lakini hakuna mazingira ya kuridhisha , pamoja na vyoo pembezoni mwa bara bara mfano uwanja wa mashuja hauna choo wananchi wanajisaidia hovyo.
Pia , amesema Manispaa ya Morogoro haina kituo cha afya cha ramani ya TAMISEMI, hivyo ameshauri kujengwe angalau vituo 3 vya kuanzia ili huduma iweze kumfikia mwananchi kwa karibu.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka Watendaji na wakuu wa idara wanapoandika taarifa zao kwenye vitabu viendane na uhalisia wa taarifa zilizopo kwenye miradi. Aidha amewataka Watendaji kila mmoja kutimiza wajibu wake na kuangalia thamani ya miradi iliyopo ili iweze kusaidia maendeleo ya vizazi vijavyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoroo, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Wajumbe wa kamati ya ushauri kuzungumzia changamoto na kutoa ushauri kwa uhuru ili yatokanayo yaweze kufanyiwa kazi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa