Hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro imeweka mpango mkakati wa kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopoteza maisha kwa kuongeza vifaa vya uchunguzi na uangalizi kwa kila mgonjwa anayeshambuliwa na magonjwa ya mishipa pamoja na moyo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema hayo katika maadhimisho ya siku ya magonjwa ya moyo Duniani Septemba 29, mwaka huu kwa mkoa wa Morogoro.
Katika maadhimisho hayo ya kimkoa , mgeni rasmi alikuwa ni mkuu wa mkoa , Dk Kebwe Stephen Kebwe ambaye aliwakilishwa na mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa alisema ,magonjwa ya moyo sasa yamekuwa ni tishio kwa wananchi na nimoja ya magonjwa yanayoongoza kuua watu wengi barani Afrika , Ulaya na Amerika kwa ujumla kutokana na kiharusi , shinikizo la damu na mshituko wa mishipa ya moyo.
Dk Lyamuya alisema , hospitali ya rufaa inatoa huduma za kliniki kila wiki ambayo hutolewa na madaktari bingwa na idadi ya wagonjwa ambao wanaohudhuria inafikia 2,500 hadi 3,000 kwa mwaka .
Pia alisema, wagonjwa wa ndani kwa maana wanaolazwa wanafikia 1,000 hadi 1,500 kwa mwaka na wanaolazwa kutokana na shinikizo la damu ni 876 kwa mwaka.
Alisema , bado zipo changamoto mbalimbali kwa wananchi ikiwa na uelewa mdogo wa magonjwa hayo juu ya kijikinga , upungufu wa wataalamu na vifaa hivyo kusababisha ongezeko la rufaa kwa wagonjwa na gharama zake.
Dk Lyamuya alishauri kuwepo kwa ongezeko la bajeti ya dawa ya maradhi ya moyo ,kuongeza wataalamu katika fani ya mishipa ikiwa na kutolewa elimu kwa wananchi jinsi ya kuepuka vichocheo vinavyoweza kusababisha maradhi ya moyo .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Morogoro, Chonjo katika hotuba yake aliwashauri wananchi wa mkoa kutambua kuwa , magonjwa ya moyo si ya kuambukizwa na yanajitokeza kutokana na mbalimbali yakiwemo ulaji usio sahihi, mazingira tunayoshi na kutofanya mazoezi ya mwili.
Hivyo aliwaomba wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara, kuepuka ulevi na kurekebisha aina ya ulaji kulingana na malekezo ya wataalamu na kuwa na tabia ya kuchunguza afya zetu mara kwa mara .
Chonjo pia aliuagiza uongozi wa hospitali ya rufaa kuwa , pamoja na siku ya maadhimisho hayo yaliyoanza Septemba 28 na kufikia tamati Septemba 29, mwaka huu suala la upimaji wa afya kwa wananchi uendelee hadi kufikia Oktoba 6, mwaka huu.
“ Leo ni maadhimisho ya siku hii ya magonjwa ya moyo duniani , lakini shughuli hii iendelee eneo la viwanja vya hospitali hiyo hadi kufikia Oktoba 6, mwaka huu ili kutoa fursa kwa wananchi wengi wa manispaa kupata huduma hii bure “ alisema Chonjo.
Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kuchunguza afya zao siku ya kilele hicho mjini Morogoro kwa nyakati tofauti walipongeza Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) , na Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha siku hiyo maalumu kwa kutoa elimu na upimaji.
Walisema , baadhi yao wameweza kuzitumia siku hizo kufika kupima na kujitambua iwapo wanazo dalili na magonjwa ya moyo au shinikizo la damu na kupewa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kujikinga nayo na kuchukua tahadhari ya mfumo wa ulaji wa vyakula na kufanya mazoezi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa