Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekabidhi shughuli za uendeshaji na matengenezo ya mradi wa Maji wa Kasanga kwa Mamlaka ya Maji na usafi wa mazingira (MORUWASA).
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Bw Ignas Sanga ameeleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kupitia Awamu ya kwanza ya Program ya maendeleo ya Sekta ya Maji(WSDP1).Lengo la mradi ni kutoa huduma ya maji safi ,salama na ya kutosha kwa wakazi wapatao 6,890 wa mtaa wa Kasanga na Mzaga ifikapo 2025.Aidha alieleza kuwa gharama za mradi ni shilingi 443,187,738.00 ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu kupitia Mfuko wa pamoja wa Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Kaimu Mkurugenzi Bw Sanga ameeleza mradi wa Maji wa mtaa wa Kasanga ulifikiwa mara baada ya wananchi wa mtaa huo kuuibua mnamo mwaka 2007 ambapo uliingizwa kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na ujenzi wa mradi ulianza tarehe 10/12/2014 na kukamilika tarehe 16/04/2016.
Akipokea mradi huo Mkurugenzi wa MORUWASA Bw Nicholaus Angumbwike ameeleza kuwa kukabidhi mradi huu kwenye Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Morogoro ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria ambapo kifungu Na.13(1) cha sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira Na.12 ya mwaka 2009 kinaelekeza kuwa Mamlaka za Maji ndio zenye dhamana ya kisheria ya kutoa huduma ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kiutawala.
Aidha Bw Angumbwike. alieleza kuwa wananchi kupitia vikao vilivyofanyika kuanzia ngazi ya mtaa mpaka ngazi ya Halmashauri kwa hiari yao waliikubalia na Halmashauri kukabidhi mradi huo kwaajili ya shughuli zote za uendeshaji na matengenezo hivyo Halmashauri haitahusika tena na uendeshaji na matengenezo ya mradi huo.
Pia ameeleza faida za mradi huo kwa wakazi wa mtaa wa Kasanga kuwa ni pamoja na kuboresha kipato cha wananchi kwa kutumia mda mfupi kupata maji safi na salama,kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama,na kujenga mazingira mazuri ya wanafunzi wa shule ya msingi ya Kasanga na shule ya Sekondari ya Bondwa ya kuwa na mda mwingi wa kujisomea badala ya kutafuta maji.
Naye Mkurugenzi huyo ameupongezaa uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuusimamia toka kuibuliwa kwa mradi huo hadi hatua ya ujenzi na hatimaye kukamilika.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa