AFISA Maendeleo ya Jamii na mratibu wa dawati la maendeleo ya watoto Manispaa ya Morogoro, Joyce Mugambi, amewataka wanafunzi wa kike kuvaa magauni manne ili waweze kutimiza ndoto zao.
Kauli hiyo, ameitoa katika hafla ya ugawaji wa taulo za mtoto wa kike zilizotolewa na Taasisi ya WEZESHA MABADILIKO kwa wanafunzi wa sekondari wanaoishi katika mazingira magumu katika ukumbi wa mikutano wa Kilakala uliopo Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza mara baada ya ugawaji wa taulo hizo, Mugambi, amesema kuwa wanafunzi wanatakiwa kusoma kwa bidii ili wafikie malengo ikiwamo magauni manne ambayo ni sare za shule, sherehe za kuagwa za kimasomo ya elimu ya Juu (graduation), Harusi pamoja na wanapoingia katika majukumu ya kifamilia ya kuwa mama ambayo ndio hatua ya mwisho wa kufikia ndoto zake.
Mugambi, amewasihi wanafunzi wasiruke hayo magauni wakaharakia kuvaa magauni kwa kuvuka hatua za uvaaji wa magauni hayo jambo ambalo litawapaelekea kutofikia malengo waliojiwekea.
“ Leo mmeona jinsi watu wanavyotambua umuhimu wenu, nanyi mnatakiwa msome kwa bidii haya magauni mkayavae kwa hatua msiruke hata hatua moja, ukiruka hatua basi ujue unakwenda kubaya, someni kwa bidii mfike chuo kikuu, mfanye sherehe zenu kama wasomi, baaada ya hapo mtaingia katika hatua ya kuwa na familia yaani ndoa kwa kupata mtu ambaye atakuwa chaguo lako na baada ya hapo utapata familia yako hapo utakuwa umekamilisha safari ya mafanikio yako” Amesema Mugambi.
“Tungehitaji kuona wanafunzi wa kike katika Manispaa yetu ya Morogoro wanajitambua, tusingehitaji kuwa na wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakakatisha masomo yao na ndoto zao, natamani watoto wa kike wa Manispaa yetu ya Morogoro suala la elimu liwe Kipaumbele chao cha kwanza” Ameongeza Mugambi.
Kwa upande wa Mkuugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako Mwakiluma,amewaomba walimu kuwasaidia wanafunzi wa kike katika elimu ya kujitambua ili iwasaidie kuepukana na vishawishi vinavyoweza kupekelekea mimba za utotoni.
Dr. Lusako, amesema si masuala yote ya yanayohusu maisha yamewekwa katika mitaala, hivyo walimu wanapaswa kusimama katika nafasi zao kama wazazi ili kile wanachotamani kuwafundisha watoto wao au ndugu zao kwa lengo la kuwalinda na tabia zisizofaa, wakifanye pia kwa wanafunzi wao wa kike ili wawasaidie wasiharibike
Naye Mkaguzi masaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Inspekta Mwanaidi Lwena, ametoa wito kwa watoto wa kike kutokubali kutumiwa kama mitaji na wazazi wao kwa kukatishwa masomo na kuozeshwa mapema, ili kukabiliana na changamoto ya mimba za utotoni katika kufikia ndoto zao.
Inspekta Mwanaidi, amesema walimu wa kike wakiwasaidia na kuwa marafiki kwa watoto wa kike ni rahisi watoto kuwaeleza matatizo yanayowakabili na amewataka wanafunzi kuwa wazi kwa walimu wao wa kike ili wasaidiwe.
Katika hatua nyingine wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwembesongo Kidato cha 3, Neema Anthony, wameiomba Serikali kuona namna ya kuwashirikisha wazazi na walezi wao katika makongamano ambayo yanatumika kutoa elimu ya masuala ya jinsia ili nao wawe na uelewa juu ya masuala hayo na kujua namna ya kuwasaidia watoto wao.
Miongoni mwa shule za Sekondari ambazo wanafunzi wao wamegaiwa taulo za Mtoto wa kike ni Mafiga, Uwanja wa Taifa, Nanenane, Tubuyu, SUA, Kingo, Kihonda Maghorofani, Mwembesongo, Kayenzi pamoja na Uluguru.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa