Naibu meya Manispaa ya Morogoro Mhe, Mohamedi Lukwele amewataka wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira yao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uharibifu wa mazingira na kuwataka kupanda miti mingi hasa katika vyanzo vya maji.
Mhe. Lukwele ametoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliofanyika nje ya ukumbi wa DDC Manispaa ya Morogoro Juni 5, 2021 mara baada ya kufanya usafi na kupanda miti katika kingo za mto Morogoro.
Akizungumza na Wananchi ,Mhe Lukwele amewataka wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji na kuwasisitiza wakulima wa maeneo ya milimani kufuata sheria na taratibu wanazopewa na maafisa wa kilimo ilikufanya kilimo hicho kuwa na tija bila kuharibu mazingira na kutokulima katika vyanzo vya maji.
Aidha,amewataka wananchi kuelimishana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mazingira na kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira na kutumia nishati mbadala ambayo haiaribu mazingira na kuathili viumbe hai.
‘’ Katika maadhimisho ya mwaka huu 2021 kitaifa tunaongozwa na kauli mbiu inayosema "TUMIA NISHATI MBADALA ONGOA MIFUMO YA IKOLOJIA" maudhui ya ujumbe huu ni kuelimisha na kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira yetu” Amesema Mhe, Mohamedi
Sambamba na maadhimisho hayo Mhe.Lukwele ametoa zawadi ya fedha na vyeti kwa washindi wa usafi kwa Kata ambapo mshindi wa kwanza ni Kata ya Mafiga ambaye amepata shilingi Laki tano,kata ya Sabasaba wamepata shilingi Laki tatu, na Kata ya Mjimkuu wamepata shilingi laki mbili na kuwataka kutumia fedha kununulia vifaa vya usafi vitakavyotumika katika kata zao.
Pia ametoa vyeti kwa Afisa Afya wa Kata ya Mafiga kwa usimamizi mzuri wa usafi,na kutoa cheti kwa kituo cha Afya Sabasaba,kikundi cha usafi Kajenjenjere na M2 smart,Cate Hotel,Benki ya NBC,shule ya sekondari Morogoro,shule ya sekondari Charlotte,Shule ya msingi Chief Albert na Carmel light.
Aidha kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro Ndg Jeremia Lubereje ambaye pia ni mchumi wa manispaa ya Morogoro ameendelea kusisitiza juu ya kushirikiana na Taasisi, wananchi wenye uelewa wa kuzifanya taka kuwa mali hususani taka za plastiki na kutengeneza bidhaa yeyote yenye kuhifadhi mazingira.
"Kudhibiti utupaji holela wa taka ngumu na usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi,sisi kama Manispaa kupitia maafisa Afya waliopo katika Kata zote tumeendelea kuielimisha jamii kuacha kutupa taka hovyo, na kupitia kampeni za usafi wa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi tumekuwa tukipita kila kata kuhamasisha usafi wa mazingira"Amesema Lubeleje.
Hata hivyo , Afisa mazingira manispaa ya Morogoro Ndg. Dawson Jeremia amesema kuwa matumizi ya nishati isiyozingatia utunzi wa mazingira umesababisha kuwepo kwa changamoto nyingine ikiwemo upotevu wa viumbe hai, uharibifu wa ardhi, upotevu wa mimea asili na , upungufu wa upatikanaji wa maji na uzalishaji hafifu wa kilimo.
Aidha, amesema kuwa mpaka sasa Manispaa imeshirikiana na wadau wa mazingira wakiwemo RELEIGH, TFS, MORUWASA, BONDE kwa mwaka huu wa fedha2020/2021 kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ambapo jumla ya miti iliyopandwa ni 15,680, Katika maeneo ya taasisi za shule na vyanzo vya maji.
Maadhimisho haya yalianzishwa mwaka 1972 katika mji wa Stockholm Sweeden kwenye mkutano wa kwanza wa umoja wa mataifa kuhusu mazingira hivyo nchi mbalimbali zimekuwa zikiadhimisha siku ya Mazingira kwa ujumbe maaluu unaotolewa na umoja wa mataifa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa