Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, mheshimiwa Ummy Nderiananga ametoa rai kwa jamii kutafakari nafasi waliyonayo katika kupinga kwa nguvu zote masuala yote na tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU), ikiwemo unyanyapaa, ukatili wa kijinsia, mila zinazochangia maambukizi, ngono katika umri mdogo, na kuporomoka kwa maadili.
Mheshimiwa Nderiananga ametoa rai hiyo leo tarehe 27.11.2023, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Nashera Morogoro, alipokuwa akifungua rasmi Kongamano la Kitaifa la Kisayansi, lenye lengo la kutathmini mafanikio, changamoto, na mwelekeo wa Taifa katika kutekeleza lengo la kutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030, pamoja na kutoa taarifa za kisayansi zitakazoboresha afua za UKIMWI nchini.
“Kama Taifa tunahitaji kuihamasisha jamii kuwa mstari wa mbele kuweza kutoa mchango wake katika kufikia azma ya kutokomeza UKIMWI kwa kuzuia maambukizi mapya hasa kwa kundi la vijana hasa wasichana ambao kwa mujibu wa takwimu, ndio wenye kiwango kikubwa cha maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hapa nchini” alieleza mheshimiwa Nderiananga.
Vilevile, mheshimiwa Nderiananga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Daktari Samia Suhulu Hassan kwa utayari na uimara wake wa kuonesha kwamba Serikali inao uwezo wa kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI hapa nchini, kwani katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya mapambano hayo na kazi inaendelea.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mheshimiwa Adam Malima amesema Sayansi imekuwa na mchango mkubwa sana katika kuwasaidia watanzania na Taifa kwa ujumla kuwa na uelewa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI kiasi kwamba hivi sasa hata wanandoa wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wanaweza kupata watoto wasio na maambukizi.
“Kwenye miaka ya 1990 ilikuwa ukipata UKIMWI ni hukumu ya kifo, na unyanyapaa ulikuwa mkubwa sana ndani ya jamii hivyo watu wengi waliokuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) walifariki kutokana na kutokuwa na uelewa wa ugonjwa huu pamoja na unyanyapaa, lakini sasa hivi Sayansi imetusaidia sana kuushinda ujinga dhidi ya ugonjwa huu” alisema Malima.
Naye mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), ndugu Mohamed Toure ametaja umasikini uliokithiri kuwa ndio kichochezi kikubwa cha maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI katika nchi za Afrika, ambapo amesema takwimu za mwaka 2022 za hali ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI duniani zinaonesha kwamba nchi za ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania, ndio zenye kiwango kikubwa cha watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), huku kundi la vijana wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 likiwa ndilo linaloongoza kwa kuwa na watu wengi wenye maambukizi hayo.
“Kati ya watu 3,600 wanaopata maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI kila siku duniani, asilimia hamsini ni kutoka kwenye ukanda wa Jangwa la Sahara, na 360 kati yao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 huku 3,200 wakiwa ni watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea na ambao kati yao asilimia 40 ni wanawake, asialimia 30 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 na asilimia 18 ni wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24” alifafanua ndugu Toure.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa