Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange (MB), ameahidi kufanya upanuzi wa miundombinu ya wodi katika Kituo cha afya cha Sabasaba kilichopo Manispaa ya Morogoro.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 18/2021 wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika Kituo hicho cha afya.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Dr Dugange, amesema ipo haja ya kituo hicho cha afya kuongezewa miundombinu ya wodi ili hata wananchi wakifika kupata huduma wapate sehemu za kulazwa kwani bado kituo hicho kina eneo la kutosha.
Dr Dugange, amesema kuwa atahakikisha suala hilo analifikisha Wizarani ili kuona ni kwa namna gani anaweza kuona miundombinu hiyo inakamilika hata kwa kuanzia kwa ujenzi wa awamu kwa awamu lengo ni kupata wodi ya kulazwa wagonjwa.
Katika hatua nyingine, Dr Dugange, ameupongeza uongozi wa Kituo cha afya chini ya Mganga mfawidhi wa kituo hicho kwa kufanya vizuri katika eneo la makusanyo ya fedha kupitia mifuko ya afya ikiwemo NHIF , CHF, pamoja na uuzaji wa dawa na huduma nyingine.
"Naamini kabisa mnanafasi kubwa ya kuendelea kukusanya fedha zaidi ya hizi mnazo kusanya kwa sasa kama mkijipanga vizuri, kwa sababu nyinyi kwa wastani kwa mwezi mnakusanya milioni 12 sawa na ukusanyaji wa shilingi 400,000/= kwa siku, kwahiyo ukijumlisha fedha za NHIF milioni 4, CHF milioni 2 na zile milioni 12 ambazo hazihusiani na mifuko hii ya afya mtajikuta mnakusanya milioni 18 kwa mwezi hivyo mnauwezo wa kuboresha mifumo zaidi mkapata kwa mwezi zaidi ya milioni 25 kama mkijipanga vizuri " Amesema Dr Dugange.
Aidha, Dr Dugange, ameutaka Uongozi huo kwa kushirikiana na Manispaa wakae chini waweke mipango mizuri ambayo kwa sasa ni agenda ya kongeza mapato mara mbili ya hapo yanayokusanywa katika Vituo husika .
Amesema kuwa Serikali kwa sasa imedhamiria kuboresha huduma za afya ili vituo vya afya viweze kuongeza wateja wengi zaidi , wateja wasikae muda mrefu kusubiria huduma
Hata hivyo, ameupongeza Uongozi wa Kituo hicho cha afya kwa kuwa na dawa za kutosha na mpangilio mzuri wa bohari ya dawa jambo ambalo linaonesha dalili nzuri ya kupata huduma bora na kuongeza wateja wengi zaidi.
Dr Dugange, ameutaka Uongozi wa Kituo hicho cha afya kuhakikisha kwamba wanashughulikia haraka sana changamoto za vifaa tiba ili viweze kutumika katika kutoa huduma kwa wateja.
Amesema kuwa kuwepo kwa changamoto za vifaa tiba kunawapotezea mapato kutokana na kuwakosa wateja wanaohitaji huduma za vipimo lakini kuna athiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi .
Mwisho amemuagiza Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha afya kuhakikisha wanawahudumia haraka Wazee ili kuendana na dhana ya Serikali ya kuanzisha dawati la kuwahudumia wazee kuliko kuwaacha wazee wakikaa muda mrefu kusubiria huduma.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa