KATIBU Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amefunga mashindano ya Umoja wa michezo kwa shule za msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa kusaidia timu zao zinazoshiriki mashindano hayo kwa kuwapatia vifaa vya michezo pamoja na kutoa michango ya ushiriki.
Hafla hiyo ya ufungaji wa mashindano hayo imefanyika Mei 29 mwaka huu katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Morogoro iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ambapo Halmashauri zote 9 za Mkoa huo zimeshiriki kwa kutoa wanamichezo.
Dkt. Mussa amesema kuwa Wakurugenzi wanajukumu la kusaidia wanamichezo wao kwa kutoa michango ikiwemo fedha za ushiriki na vifaa vya michezo kwa mashindano yajayo hivyo wakurugenzi wajipange kikamilifu.
“...lakini mbaya zaidi hata hao wanafunzi wanaokuja kuwakilisha Halmashauri zenu mmeshindwa kuwapa sare nzuri sasa mimi niwaambieni hili sitaki kuliona tena kwenye michezo ijayo...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Katibu Tawala huyo amesema michezo ina faida nyingi sio kuimarisha afya bali hupanua uwezo wa akili kufikiri, pamoja na kupunguza matukio ya kiharifu kwa sababu watu watatumia muda mwingi kwenye michezo kuliko kukaa vijiweni bila kazi.
Sambamba na hilo Dkt. Mussa amewatakia kila la heri wanamichezo waliochaguliwa kuuwakilisha Mkoa katika Mashindano hayo ngazi ya Taifa yatakayofanyika Juni 2, 2023 Mkoani Tabora na kuahidi kuandaa zawadi endapo timu hiyo itafanya vizuri katika mashindano hayo.
Awali, Afisa Michezo Mkoa wa Morogoro Bi. Grace Njau amesema mashindano hayo yamewakutanisha wanamichezo 938 kutoka Halmashauri zilizopo Mkoa wa Morogoro wakiwemo wavulana 453, wasichana 485 ambao wameshiriki michezo mbalimbali ikiwemo michezo ya riadha, mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, kwaya, na muziki.
Bi. Grace ameongeza kuwa mashindano ya mwaka jana Mkoa wa Morogoro ulishika nafasi ya tano kitaifa, pia ulipata Medali nne katika mashindano ya Afrika.
Mashindano hayo kwa mwaka huu yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Uimarishaji wa miundombinu ya elimu nchini ni chachu ya taaluma, sanaa na michezo”.
Jumla ya wanamichezo 102 wamechaguliwa kuuwakilisha Mkoa katika mashindano hayo ya UMITASHUMTA ngazi ya taifa Mkoani Tabora ambayo yataanza Juni 2 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa