Wafanyakazi na watumishi wa Umma Mkoa wa Morogoro,wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kujiepusha na masuala ya rushwa na utovu wa nidhamu kazini.
Rai hiyo imetolewa Mei 1/2021 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,Mhandisi Emmanuel Kalobelo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. LoataSanare, katika maadhimisho ya Siku ya sherehe za Mei Mosi katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Jamhuri.
Kalobelo,amesema kuna baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakikiuka maadili ya kazi na taaluma zao na kujikuta wakiwa watovu wa nidhamu na kujikita kwenye masuala ambayo yako kinyume na utaratibu wa kazi hivyo ni vyema kwa kila mfanyakazi akazingatia maadili ya kazi zake.
Aidha, amesema kuwa risala iliyoandaliwa ameipokea na kuifikisha katika ngazi za juu za uongozi huku akiwataka wafanyakazi kuwa wavumilivu katika kazi na wawe na matarajio makubwa na Serikali yao katika suala zima la stahiki zao ikiwemo kuongezwa mishahara pamoja na kupanda kwa madaraja kazini.
Kuhusu madeni ya wafanyakazi, amesema kuwa Serikali inaendelea kushughulikia madeni ya Watumishi wa Umma, hivyo Serikali mara itakapomaliza kuingiza madeni yote katika mfumo madeni hayo yatalipwa.
"Madeni yanayolipika hayatakiwi kufika katika orodha ya madeni ya muda mrefu, hivyo nawaagiza viongozi wa taasisi wakayachuje madeni hayo , nitafanya ukaguzi wa madai ya Wafanyakazi kuona jinsi yanavyofuatiliwa, tunakuwa na madeni makubwa kumbe ukiyachunguza utakuta wapo wafanyakazi wanadai pesa ndogo tu hizi zilipwe , tukilipa madeni madogo tunaweza kubaki na madeni makubwa lakini nazionya pia Taasisi zinazozalisha madeni kilazima" Amesema Eng. Kalobelo.
Amesema kuwa maslahi bora ya Wafanyakazi huongeza ufanisi mahala pa kazi na kupunguza migogoro kazini, huku akiwaagiza waajiri wote wa Mashirika ya Umma na binafsi kuweka Mazingira wezeshi kwa Wafanyakazi ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo jambo ambalo litapunguza migogoro, na kuongeza ufanisi kazini.
Hata hivyo katika kuona wafanyakazi wanapata sehemu ya kuyasemea matatizo yao, amewakumbusha waajiri kuwaunganishaWafanyakazi katika vyama vya Wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ofisi za Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya mashariki , huku akiitaka Ofisi ya Afisa Kazi Mkoa wa Morogoro kupitia na kufanya ukaguzi kwa Makampuni ambayo hayana mikataba na wafanyakazi na kuangalia mikataba ambayo imepitwa na wakati inayokandamiza haki za wafanyakazi.
Kuhusu maboresho ya mikataba ya wafanyakazi, amesema kuwa mikataba mingi ya Wafanyakazi imepitwa na wakati hivyo waajiri wazingatie kuiboresha mikataba hiyo huku wakishirikiana na viongozi wa vyama vya Wafanyakazi.
Hata hivyo mara baada ya kugawa zawadi za wafanyakazi hodari, amewataka wafanyakazi wote waviishi vigezo vya wafanyakazi hodari ili wafanyakazi wote wawe bora ili kuchangia maendeleo kwenda kwa kasi.
Wakati huo huo, amesema ni vyema wafanyakazi wakaongeza bidii na uzalishaji mali ili Taifa la Tanzania liweze kufikia uchumi wa juu na kuliletea Taifa maendeleo, huku akiipongeza Serikali kwa kudhibiti mfumuko wa bei wa vyakula na bidhaa.
Katika hatua nyingine, amewataka waajiri kuanza kutoa mafunzo mapema ya wastaafu wanapokuwa kazini badala ya kusubiria wamebakiza mwaka mmoja ndio watoe mafunzo ya wastaafu jambo ambalo halina afya sana kwa wastaafu kutokana na kuchelewa kupata elimu ya ujasiriamali.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Morogoro, (TUCTA), Mohammed Simbeye, amemuomba Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa karibu mashirika yenye nia ya kuchafua jina la Mkoa kwa kuzuia haki za wafanyakazi ikiwemo kuanzisha vyama vyao wakiwa katika maeneo yao ya kazi.
Simbeye, amemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kuwasukuma waajiri katika Mashirika mbalimbali yaliyoko Mkoani Morogoro iliwasajiri wafanyakazi wao katika mifuko ya bima ya Afya bila kujali kipato anachopata mfanyakazi husika.
Sherehe ya siku ya wafanyakazi hufanyika kila ifikapo Mei Mosi ya kila mwaka ikiwa na lengo la kutathmini mwenendo na hali za wafanyakazi ikiwa sambamba na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wafanyakazi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2021 ni" Maslahi bora, mishahara juu kazi iendelee".
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa