Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi. Emmanuel Kalobelo, amewataka wakina mama Wajasiriamali kuibua miradi yenye tija na inayotekelezeka ili kuweza kurejesha fedha za mikopo kwa wakati kuliko kuwa na biashara ambazo haziwezi kuwapatia faida kwa wakati.
Ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yaliyofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Jamhuri Machi 8, 2020.
Akizungumza na Wakina Wanawake waliojitokeza katika Maadhimisho hayo, amesema Wajasiriamali wanapaswa kubadilika na kubuni biashara kubwa ambapo watakopeshwa vifaaa badala ya fedha kwani Serikali ipo tayari kuwawezesha kununua Vifaa na mashine za kuendeshea shughuli zao za uzalishaji.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli , imepitisha Sheria ya utoaji wa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu na kutengeneza kanuni za uendeshaji wa mfuko wa mkopo, ambapo sheria hiyo imeelekeza kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ili kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi ya wanawake asilimia 4, Vijana asilimia 4 na Watu wenye Ulemavu asilimia 2.
Pia amesema zoezi la utoaji wa vyeti vya pongezi lililofanywa na Manispaa ya Morogoro litakuwa endelevu kwa kutoa vyeti na tuzo mbalimbali kwa Vikundi vinavyofanya vizuri.
Amesema Vikundi vya Wajasiriamali vinatambua nia ya Serikali ya kukopesha Wajasiriamali wadogo ambao wanakosa fursa za kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki.
“Wakinamama pamoja na Wajasiriamali nawapongeza wote kwa juhudi za uzalishaji mali na mshikamano mnaouonesha katika kujenga Halmashauri yenu hususani katika suala zima la maendeleo, hii imepelekea Halmashauri yenu kusonga mbele katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ambayo inavutia na kuweza hata Halmashauri nyingine kuja kujifunza kwenu hongereni sana, nimetoa hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni 100,000,000 mnatakiwa fedha hizi kuzitumia kwa malengo, mjitahidi kuwa waaminifu na kurejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vyingine ”. Amesema Kalobelo.
“Kuna vikundi ambavyo vimefanya vizuri sana na vimerejesha mikopo kwa wakati na wanastahili pongezi, nami nichukue fursa hii kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha lakini pia mmeonesha uaminifu katika matumizi ya fedha hizi za mkopo, ni dhahiri mmeweza kuongeza na kukuza mitaji yenu hata mkaweza kurejesha kwa wakati, wengine wote ambao bado mnadaiwa mjitahidi kurejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine waweze kunufaika na mkopo huu, ni kuombe Mkurugenzi wa Manispaa uendelee kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ili muwakopeshe wajasiriamali hawa wanaotafuta mitaji ya kukuza biashara zao ” Ameongeza Kalobelo.
Amesema kuwa ili kuleta mapinduzi yaliyo ya kweli na ya Kimaendeleo lazima uwekezaji ufanyike kwenye shughuli zinazoendana na na uanzishwaji wa Viwanda, kama sera ya nchi inavyoelekeza aliyoionyesha Mhe. Rais Dkt John Magufuli ya kauli mbiu ya hapa kazi tuu na kumuunga mkono kwa kutekeleza kwa vitendo ambapo katika awamu hii wanawake wamepewa nafasi kubwa kama nguvu kazi , wazalishaji na walezi wakubwa katika familia na kuwaomba wasimuangushe Mhe. Rais wafanye kazi kwa bidii na kuweka mikakati mizuri ya uzalishaji mali kwa kushirikiana na wanaume zao kuanzia ngazi ya familia na kusongesha Taifa mbele kiuchumi.
Aidha , amewataka Wanawake waangalie maendeleo ya familia zao kwa ujumla katika Nyanja zote kwani usawa au kutokuwa na usawa chimbuko lake linaanzia katika ngazi ya familia ambapo mfumo dume unazaliwa na kuendelezwa.
Amesema ni muhimu wanawake wakashirikiana kwa pamoja na wanaume zao katika suala zima la malezi katika familia zao ili kujenga kizazi kinachozingatia usawa kuanzia watoto wakiwa wadogo hadi watakapokuwa watu wazima na hii itasaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu wanayoyatarajia.
Pia amechukua fursa ya kuwakumbusha wakina mama waendelee kukemea vitendo vay ukatilia wa kijinsia vinavyoendelea katika jamii.
Pia amesisitiza ushirikiano wa kamati za kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika ngazi za mitaa, Kata hadi Manispaa kushirikiana na Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia katika kutoa elimu ya masuala ya ukatili na kutoa taarifa za matukio ya ukatili yanayofanyika katika maeneo yakiwemo ubakaji na ulawiti ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wanaotenda makosa hayo.
Amesema ukatili wa jinsia una madhara makubwa kwani unasababisha ulemavu wa kudumu, maambukizi ya Virusi vya UKIMWI athari ya kisaikolojia kwa watoto na hatimaye kurudisha nyuma maendeleo kwa mhanga wa ukatili.
Ametoa wito kwa wanawake na kuwaeleza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli, imeanzisha programu mbalimbali ikiwamo programu ya Elimu bure, Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF), na mkakati wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kuagiza idara zote zinazohusika na programu hizo kuhakikisha wanasismamia huduma hizo ipasavyo na kuwaasa wanawake kupitia mikutano yao ya vikundi vya kijamii kama vile VICOBA, SACCOS wapeane taarifa za kimaendeleo na wawe tayari kuhudhuria mikutano ya Mitaa inayoandaliwa kwa mujibu wa sheria kwani huko ndiko chimbuko la taarifa za kimaendeleo na fursa mbalimbali zinazojitokeza.
Pia amewataka wataalamu na Viongozi wa Manispaa kuhakikisha wanawatumia wenyeviti wa Mitaa vizuri na ikiwezekana uhamasishaji ufanyike nyumba kwa nyumba ili wananchi wajiunge na CHF , Watoto chini ya miaka mitano waandikishwe na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Hata hivyo amewataka wakina mama wajitokeze kwa wingi katika kipindi cha uchaguzi mkuu Oktoba 2020 ili waweze kugombea nafasi za Uongozi katika maeneo yao jambo amabalo litadhihirisha kwamba wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya “KIZAZI CHA USAWA KWA MAENDELEO YA TANZANIA YA SASA NA YA BAADAYE” huku akiwapongeza wanawake wote waliojitokeza katika kugombea nafasi uchaguzi wa Serikali za Mitaa na waliojitokeza katika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema Manispaa ya Morogoro inatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na wajasiriamali wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 manispaa imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya mikopo ambapo kati ya hizo shilingi milioni 45,5000,000.00/= zimetolewa kwa vikundi 9 vya Wanawake, shilingi milioni 45,500,000.00/= kwa vikundi 11 vya Vijana na shilingi milioni 9,000,000.00/= kwa vikundi 3 vya watu wenye ulemavu.
Ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo katika kusukuma gurudumu mbele la maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro huku akiwataka wanawake na wakina mama pamoja na vijana wale waliokuwa majumbani wajiunge na vikundi ili waweze kupatiwa mikopo na kujikwamua kiuchumi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 , Halmashauri ya Manispaa Morogoro ilitoa mkopo wa Shilingi Milioni 402,500,000/= kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ambapo vikundi 76 vya wanawake vilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 214,500,000/=, vikundi 51 vijana walipewa shilingi milioni 151,500,000/= na vikundi 13 vya watu wenye ulemavu walipewa shilingi milioni 36,500,000/=.
Amesema mpaka kufikia Oktoba 2019 vikundi 22 vya wanawake vilipaswa viwe vimekamilisha marejesho , vikundi 12 pamoja na vikundi 11 vya watu wenye ulemavu vyote vilipaswa viwe vinaelekea katika kurejesha fedha.
Amesema Manispaa ya Morogoro kupitia muunganiko wa wanawake wajasiriamali vya jukwaa linaendesha darasa la ushonaji eneo la Tushikamane ambapo hadi sasa jumla ya wanafunzi 20 wamemaliza awamu ya kwanza ya ushonaji waliobaki ni wanafunzi 3 na kituo kinaelekea kusajili wanafunzi wengine.
Amesema kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 kuanzia Julai hadi kufikia mwezi Februali jumla ya vikundi 205 vimesajiliwa na kati aya hivyo vikundi viwili vya Vijana vimeshapatiwa mkopo mna Manispaa.
Katika maadhimisho hayo miongoni mwa shughuli zilizokuwa zikifanyika ni pamoja na Maonesho ya bidahaa mbalimbali za wanawake zinazofanywa na wajasiriamali pamoja na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau , Elimu ya Jinsia na ukatili kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari, Huduma ya Msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji katika Kata ya Lukobe na Kata Jirani za Kihonda na Mkundi, Utoaji wa msaada kwa kituo kimoja cha watoto yatima kituo cha Mgolole, kambi ya Wazee Fungafunga, Gereza la wafungwa wanawake Kingolwira na kwa watoto wenye ulemavu wa akili kituo cha Mehayo Kata ya Mazimbu, Upimaji wa Saratani ya shingo ya kizazi na VVU , Bonanza kwa Wananchi wa Mzinga na uchangiaji wa damu salama pamoja na Mashindano ya michezo kwa wanawake ikiwemo kukimbiza kuku, kukimbia kwenye gunia na kuvuta kamba.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa