Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ally Mussa ameshirikiana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro mheshimiwa Pascal Kihanga kugawa miche zaidi ya elfu nne (4,000) ya mikarafuu kwa viongozi wawakilishi wa wananchi wa Kata za Bigwa, Kilakala, Magadu, Luhungo, Boma na Mlimani.
Akizungumza na wenyeviti wa mitaa, wajumbe, wakulima na baadhi ya waheshimiwa madiwani kabla ya ugawaji wa miche hiyo kwenye uwanja wa Ofisi za Kilimo za Manispaa ya Morogoro, Dkt. Mussa amemshukuru Mstahiki Meya pamoja na menejimenti ya Manispaa kwa kuridhia kununua miche ya karafuu na kuigawa bure kwa wananchi wa Kata za milimani ikiwa ni jitihada za makusudi za Manispaa kuhakikisha uhifadhi wa mazingira katika milima ya Uluguru.
Dkt. Mussa amewataka wananchi wote watakao gawiwa miche hiyo wahakikishe wanaipanda na kuitunza kwa sababu mikarafuu haitasaidia kutunza mazingira peke yake bali itakapo zaa itakuwa ikivunwa na kuuzwa na hivyo itakuza pato la wananchi.
“Jamani hii miche ni mali. Hakikisheni mnaipanda kwa wingi na kuitunza ili ikue. Leo miche zaidi ya elfu nne itakabidhiwa kwenu lakini tunayo ahadi ya miche elfu 30 kutoka kwa watu wa bonde, na yote hiyo ni kwa ajili yenu.
“Tunafanya yote haya kuhakikisha tunaunga mkono jitihada za rais Samia za kuinua pato la wananchi. Manispaa yetu imedhamiria kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wake ndio maana inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kununua miche ya mikarafuu na kuigawa bure kwa wananchi” alieleza Dkt. Mussa.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro mheshimiwa Pascal Kihanga amesema, lengo namba moja la Manispaa kukubali kujaza miche ya mikarafuu kwenye milima ya Uluguru ni kutunza mazingira ya milimani.
“Nataka watu wa milimani mjue kwamba kama Manispaa tumeshaamua kwamba hamtahama huko milimani kupisha uharibifu wa mazingira, badala yake tunataka mpande miti ya mikarafuu maana itasaidia sana kuyahifadhi mazingira na kuwaweka ninyi salama.
Nao viongozi wawakilishi wa wananchi wa Kata za milimani miongoni mwao wakiwemo waheshimiwa madiwani, wamemshukuru sana Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Mussa Ally Mussa kwa kuleta njozi hii njema ndani ya Manispaa, na wameahidi kuwasimamia wananchi wote watakaopewa miche, wanaipande na kuitunza.
Leo ni awamu ya pili ya mgao wa miche ya mikarafuu kwa wananchi, awamu ya kwanza jumla ya miche elfu mbili (2,000) itolewa.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa