MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Morogoro una fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumiwa vizuri uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla utakua.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Juni 1/2023 kwenye hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Fatma Mwassa katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema pamoja na Mkoa huo kushika nafasi ya kwanza kwenye uzalishaji wa chakula hapa nchini lakini kuna haja ya Mkoa kuweka mikakati bora ili kuhakikisha kuwa Mkoa unashika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa Chakula.
"...tunaenda kujadiliana pale ambapo tunakuwa mtu wa tano au wa nne, kwa nini tusiwe wa kwanza, kinachotukwaza tusiwe mtu wa kwanza ni nini?..." amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Adam Malima amesema mifugo ya Morogoro lazima iwe na mchango kiuchumi ndani ya Mkoa na Taifa kwa jumla vinginevyo kitakuwa hakuna maana.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Mkoa amemuhakikishia Mhe. Fatma Mwassa kuwa ataendeleza mazuri aliyoyaacha katika Mkoa huo pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali.
Awali, Mhe. Fatma Mwassa ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera amemuhakikishia Mhe. Adam Malima kupata ushirikiano kutoka kwake ili kufanikisha harakati za kuwaletea wanamorogoro maendeleo.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo amemshukuru Mhe. Fatma Mwassa kwa uongozi wake uliotukuka katika kuhakikisha kuwa viongozi ndani ya Mkoa huo wanakuwa na maono ya pamoja.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa