Vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kuongezeka siku kwa siku ndani ya mkoa wa Morogoro lakini Kamati ya Usalama ya mkoa imeshaanza kuandaa mkakati kabambe wa kuvidhibiti na ikibidi kuvitokomeza kabisa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mheshimiwa Adam Kighoma Malima alipokuwa akizungumza na wananchi wa mkoa huo, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 08 mwezi wa tatu.
Mheshimiwa Malima amewataka wanawake, ambao ndio kundi linaloonekana kuathiriwa zaidi na vitendo hivyo kuliko wanaume, kutokaa kimya pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili badala yake wapeleke taarifa kwenye Dawati la Jinsia la Polisi, ama kwenye Ofisi za Ustawi wa Jamii ili kuweza kupata msaada wa kisheria.
Pia, ameitaka Mahakama pamoja na Taasisi zinazoshughulika na masuala ya haki za binadamu, kuongeza kasi katika kutoa elimu ya aina za ukatili wa kijinsia na haki za akina mama waliomo katika mifumo ya ukatili wa kijinsia.
Mbali na ukatili wa kijinsia, mheshimiwa Malima amewapongeza wanawake kwa kuwa warejeshaji wazuri wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmshauri mbalimbali nchini ukilinganisha na kundi la vijana na watu wenye ulemavu ambao pia hunufaika na mikopo hiyo.
Aidha, mheshimiwa Malima amempongeza Rais Samia kwa kuwa mfano wa kuigwa na wanawake wote ndani na nje ya Tanzania, jambo linalopelekea wanawake wakiwemo wa mkoa wa Morogoro kuendelea kutoa michango yao kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wao wanawake wa mkoa wa Morogoro ambao sauti zao ziliwasilishwa kupitia Risala iliyosomwa mbele za Mkuu wa Mkoa, wamemshukuru Rais Samia kwa kujenga shule za bweni maalum kwa ajili ya watoto wa kike kwenye mikoa mbalimbali nchini na mkoa wa Morogoro ukiwa miongoni mwayo kwani jambo hili linaonesha jinsi gani Serikali inapamabana kuwekeza kwa mwanamke ili kuharakisha maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii kwa ujumla.
Mwisho, wameiomba Serikali iongeze jitihada katika kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo yote nchini kwa kutunga sheria zitakazo wabana wale wanaojihusisha na vitendo hivyo.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa