Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima, amewahimiza wananchi wa mkoa huo na wa mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye shughuli zote zinazoendelea kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Morogoro, ikiwemo kupata huduma za upimaji wa afya na kupata elimu ya VVU na UKIMWI itakayokuwa ikitolewa kila siku na wadau mbalimbali, katika kipindi chote cha wiki ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani.
Mhehsimiwa Malima ameyasema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, uzinduzi uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Morogoro leo tarehe 24.11.2023, ambapo pia alisema kwamba baada ya maadhimisho hayo, kama Mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla tutafikia malengo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS), ya kuwa na sifuri tatu ambazo ni sifuri ya maambukizi mapya ya VVU, sifuri ya vifo vitokanavyo na maambukizi ya VVU na UKIMWI na sifuri ya unyanyapaa.
Vilevile, katika hotuba yake hiyo, mheshimiwa Malima amesema, Mkoa wa Morogoro mpaka sasa umefanya juhudi kubwa sana katika kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI, kwani katika vituo 629 vya kutolea huduma za afya vilivyopo ndani ya mkoa, vituo 516 vina uwezo wa kutoa huduma za VVU na UKIMWI, vituo 359 vinatoa huduma ya kupima VVU, vituo 112 vinatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU, na vituo 368 vinatoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama mwenye VVU kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na wakati wa unyonyeshaji.
Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini (NACOPHA), ndugu Emmanuel Msinga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini kuendelea kupata bure dawa za kufubaza virusi (ARV’s), na kutoa mikopo kwa vikundi wezeshi vya watu hao ili kuwasaidia kuondokana na umaskini ambao wakati mwingine unasababishwa na unyanyapaa katika jamii zinazowazunguka.
Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya, ndugu Zeye Nkomela, amesema Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za VVU kwa watu wanaoishi na maambukizi na kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI”, Wizara inaamini kwamba kufikia mwaka 2030 Serikali itakuwa imefanikiwa kufikia malengo ya kutokomeza maambukizi ya VVU nchini.
Aidha, Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani inaenda sambamba na Kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia yenye kaulimbiu isemayo “Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia, ambayo pia imezinduliwa rasmi leo na kilele chake kitakuwa tarehe 10.12.2023, ikiwa na lengo la kusisitiza jamii kuwekeza zaidi katika kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwa kuwa ndilo kundi linalosadikiwa kupitia changamoto zaidi za vitendo vya ukatili.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa