Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watendaji wa mitaa, vijiji, kata na wakuu wa idara ambao wamesababisha kuzalisha hoja za ukaguzi ama kushindwa kuwashilisha fedha za makusanyo ya ushuru wa mapato benki.
Dk Kebwe alitoa agizo hilo katika hotuba yake juzi kwenye kikao cha Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa Fedha wa 2017/2018 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Pia amesikitishwa kuona Halmashauri ya Kilombero na Ulanga kupata hati zenye mashaka na hivyo kupoteza sifa ya kupata fedha toka serikali kuu za miradi ya maendeleo ya kimkakati kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
“ Mkoa una Halmashauri tisa za wilaya , lakini mbili zimetuangusha , ni Ulanga na Kilombero na hapa hatua kali zitachukuliwa kwa waliohusika kuzifikisha hapo zilipo” alisema mkuu wa mkoa na kusisitiza.
“ Sasa ninaagiza kwa wakurugenzi wote wa Halmashauri za mkoa huu na wenyeviti wa halmashauri chukueni hatua kali za kinidhamu na za kisheria kwa haraka wote waliosababisha kuzalisha hoja za ukaguzi wakiwemo na wasiowasilisha benki fedha za makusanyo ya ushuru” alisema Dk Kebwe.
Alisema, mara nyingi hoja za ukaguzi hazijalishiwi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali , bali na baadhi ya watendaji wa halmashauri husika wasio waaminifu kuanzia wa mitaa, vijiji pamoja na wakuu wa idara kwa kushindwa kutimiza majukumu waliyopewa kuyasimamia.
Hata hivyo alizitaka Halmashauri za wilaya hizo pamoja na Manispaa ya Morogoro kuzifanyia kazi kwa kujibu hoja zote za ukaguzi kwa wakati na pia kusimamia utekelezaji wa maagizo ya kamati za Bunge .
Naye Mkaguzi mkuu wa Nje wa mkoa a Morogoro, Mwabwanga Peter akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha wa 2017/2018 alisema ,katika halmashauri saba nchini zilizopata hati zenye mashaka, mbili ni za mkoa wa Morogoro ambazo ni Ulanga na Kilombero.
Hata hivyo aliipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kupata hati inayoridhisha (hati safi ) kwa miaka saba mfululizo na hivyo kuitaka itekeleze maagizo yote kamati ya Bunge ili hoja zilizojitokeza ziweze kufutwa kwa mujibu wa sheria.
Mbali na hayo aliitaka Manispaa kuanza kujipanga kuweka mifumo mizuri na madhubuti ya usimamizi wa miradi ya kimkakati ikiwemo stendi ya mabasi ya Msamvu na Soko kuu baada ya kukamilishwa ujenzi wake ili iwe endelevu kuleta faida kwa wananchi na kuepuka kuzalisha hoja za ukaguzi kipindi cha uendeshaji .
Kwa upande wake , Meya wa Manispaa , Pascal Kihanga pamoja na kumshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa soko la kisasa ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 41alisema ,huo ni ukombozi kwa Manispaa ya Morogoro kuekelea kujitegemea kiuchumi.
“ Tukikabishiwa stendi ya mabasi ya Msamvu ambayo Rais aliagiza na pia kukamilika kwa ujenzi wa soko kuu la kisasa pamoja na miradi mingine ya kimkakati itakayojengwa , halmashauri yetu itakuwa na uchumi wenye kuimarika ambao utachangia kukuza shughuli za maendeleo ya wananchi “alisema Kihanga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa