MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa, amewaagiza Viongozi wa Halmashauri kufanya ziara za kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri viongozi wa Serikali ya mkoa ndio wazitatue changamoto za wananchi.
Ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi Kata ya Kihonda, uliofanyika Septemba 13/2022 katika eneo la Ofisi ya Kata ya Kihonda .
RC Mwassa, amesema Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawajui kinachoendelea kwasababu viongozi ambao wanapaswa kuwaeleza hawafanyi hivyo.
"Ni muhimu mno kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero zao, wahamasisheni Madiwani, makatibu tarafa wafanye ziara, mkoa wetu umekuwa ukipata fedha nyingi za miradi ya maendeleo ni wajibu wetu kama viongozi kuzisimamia ili zilete tija katika maendeleo," Amesema RC Mwassa.
Aidha, amesema kuwa kusikiliza ni moja ya uwajibikaji bora kwa wananchi, hivyo kutofanya mikutano ya hadhara kwa wananchi kuna sababisha kuibuka kwa kero nyingi ambazo kama ziara zingekuwa zinafanyika hali hiyo isingejitokeza.
Katika hatua nyingine, amepiga marufuku Watendaji wa Kata na Mitaa na wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutojihusisha na uuzaji wa ardhi, kwani kufanya hivyo kuna pelekea kuwa na mlundikano wa migogoro ya ardhi kila uchwao.
Hata hivyo, RC Mwassa, amewaagiza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri kwa kushirikiana na wataalam wa ardhi kufuatilia migogoro yote ya ardhi na kuipatia ufumbuzi na kuiweka kwenye 'data base'.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa yote aliyoyaagiza atayafanyia kazi kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa.
RAS Mussa, amewataka Watumishi wa Umma kuhakikisha kila mtumishi awe na sheria ya Serikali za Mitaa ambayo sheria hiyo ndio inayoonesha majukumu yao kwa ujumla katika kuwatumikia wananchi.
"Mkasome sheria za Serikali za Mitaa, lakini kila mtumishi awe na Ilani ya CCM inayoelekeza mambo ya kufanya , pia tuangalie maelekezo ya mkoa yanataka nini , tujenge utamaduni wa kuwajibishana ili mifumo ifanye kazi , kwa kufanya haya tunaamini kabisa tutaweza kufikia viwango vya juu vya utendaji " Amesema RAS Mussa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa