Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro kuhakikisha inawachukua wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2019 ambao wanatakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka ujao.
Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo Oktoba 24 alipofanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Manispaa ya Morogoro ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari ya Kola hill na Kingalu,ujenzi wa Soko Kuu na Stendi ya daladala iliyopo kata ya Mafiga.
Akipokea taarifa za ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika kila shule hizo,ilielezwa wananchi walihamasishwa kujenga maboma,Halmashauri ilichangia kiasi cha Tsh 2,565,000 sawa na asilimia 7 na Serikali kuu ilitoa fedha kiasi cha Tsh 25,000,000 kwa kila shule kwaajili ya umaliziaji wa vyumba hivyo vya madarasa.
RC Sanare akitoa pongezi kwa shule hizo kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo,amewashukuru wananchi kwa kujitolea kwao na kumshukuru Mhe Rais Dkt John P.Magufuli kwa kuendelea kuona umuhimu wa elimu na kuamua kutoa fedha kwaajili ya umaliziaji wa madarasa hayo.
"Manispaa ina upungufu wa madarasa 33,hivyo mnapaswa kujipanga vizuri kumaliza upungufu huo ili kila mtoto aliyefaulu aweze kuchukuliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza ifikapo mwezi Januari" Alisema Ole Sanare.
Akitotoa ufafanuzi Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba ameeleza kuwa Halmashauri imejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto hiyo ya upungufu wa madarasa na imetenga bajeti ya Tsh Mil 160 kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,pia atafanya harambee na wazazi watahamasishwa kuchangia ujenzi hivyo alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu.
Aidha RC Sanare ameendelea kusisitiza ofisi ya mhandisi kuweka sawa suala la miundombinu ya umeme katika vyumba hivyo vya madarasa,na kuendelea kufuata miongozo ya Serikali katika ujenzi wa majengo hayo na mengine.
Pia RC Sanare ametoa pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule ya sekondari Mjimpya na Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa