Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, amewapongeza wadau kwa kufanikisha ukarabati wa madarasa chakavu katika shule ya Msingi Mji Mkuu iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya ,Morogoro.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa ukaguzi wa madarasa Manne chakavu yaliyokarabatiwa chini ya ufadhili ambapo madarasa mawili yametokana na ufadhili wa Mhe. Abdulaziz Abood Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia mfuko wa jimbo na mengine mawili chini ya ufadhili wa Nashela Hotel.
Katika ukarabati wa madarasa hayo , Mfuko wa Jimbo la Morogoro Mjini uliweza kuchangia shilingi Milioni 3 na laki 6 na fedha binafsi kutoka kwa Mhe. Abood ni shilingi Milioni 1 na Laki 4 huku ufadhili wa Nashela Hoteli ukitumia takribani shilingi Milioni 10.
"Napenda kutoa pongezi zangu za shukrani kwa wadau wote, haswa Mhe. Abood na Nashela Hotel, kwakweli shule hii ipo barabarani njiani kabisa nilipiga kelele lakini leo angalau ilifikia wakati nikamwambia Mkuu wa Wilaya tuifunge shule hii wanafunzi na walimu tuwahamishe lakini sasa inaonekana kufufuka , niombe Manispaa iangalieni shule hii kwa jicho la huruma ikiwezekana tafuteni pesa haraka kukoa jahazi hali sio nzuri viongozi wanapita njia hii ni aibu kubwa " Amesema Sanare.
Amesema mikakati yake ni kuhakikisha Watoto wote waliofaulu wanaenda shule na wanakaa kwenye madawati na atazunguka kila kata kuona hali ilivyo.
Pia ameendelea kusisitiza kwamba wale walimu Wakuu waliodumu muda mrefu bila ya matokeo mazuri ya ufaulu watashushwa vyeo na kuwa walimu wa kawaida.
Aidha , amesema Walimu ambao hawako shuleni bila taarifa za msingi wakatwe mishahara yao pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Pia amewaagiza Maafisa elimu wasaidiane na Wadhibiti ubora wa elimu ili kuleta matokeo chanya ya viwango vya ufaulu katika Mkoa wa Morogoro.
"Tunachotaka ni matokeo, yapo malalamiko mengi shuleni wananchi wanaonewa wakati Serikali ilishatoa maelekezo lakini hayatekelezwi, hivyo hatutakuwa tayari kuwaadhibu wadhibiti ubora wakati wapo waratibu wa elimu, niwaombe waratibu wa elimu wasimamie shule na sitotaka kusikia malalamiko kwani kikwazo cha kwanza katika kuchangia matokeo mabaya ya elimu ni watendaji "Ameongeza RC Sanare.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ameuagiza uongozi wa Kata ya Mji Mkuu kuhakikisha wanaitisha Vikao vya kuongea na Wananchi wao kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya elimu na katika vikao hivyo wawashirikishe Mkuu wa Wilaya, Meya na Mkurugenzi ili watoe hamasa.
Amewataka waalimu na watendaji kuhakikisha kila mtu anafanya majukumu kwa nafasi yake huku akiwataka watendaji pamoja na maafisa elimu kuhakikisha kila kinachoingia na kutoka wakisimamie kwa misingi ya sheria na kanuni.
Katika ukarabati wa madarasa chakavu , utengenezaji huo ulihusisha marekebisho ya sakafu, ukarabati wa kuta za ndani na nje (plasta), ubadilishaji wa silingi bodi (ceiling board), kenchi, uezekaji wa paa jipya, upigaji rangi wa madarasa mawili, wiring na umeme kwenye madarasa mawili pamoja na taa za kuongeza ulinzi mbele na nyuma ya madarasa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa