MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amewaonya Watendaji kuacha tabia ya kuvutana na kupelekea kukwamisha miradi ya Maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 30, 2020 katika kikao cha kutatua mgogoro ulioibuka katika Ujenzi wa Madarasa na Jengo la Utawala katika Shule ya Sekondari SUA iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika kikao maalumu kilichowakutanisha, Wajumbe wa Mabaraza mawili ya Kamati za Maendeleo kutoka Kata ya Magadu na Mbuyuni, wahandisi , pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara , waalimu pamoja na Uongozi wa Shule ya Sekondari SUA, RC Sanare, amewataka viongozi hao kutoa taarifa katika ofisi husika kuhusiana na changamoto za utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Aidha , ameshangaa kusimama kwa Ujenzi wa Jengo la Utawala pamoja na Ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari SUA huku akiwataka Watendaji kufuata mifumo ya kiutawala na kuacha tabia ya kuvutana kwa maslahi yao binafsi na sababu zisizo na msingi .
Kuhusiana na ujenzi unaosuasua wa madarasa pamoja na Jengo la Utawala katika Shule ya Sekondari SUA, ametoa muda wa wiki mbili kukamilisha ukarabati wa ujenzi wa Madarasa na miezi miwili kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Utawala.
"Nimekuja hapa baada ya kusikia kuna mvutano wa fedha baina ya kata hizi mbili yani Magadu pamoja na Mbuyuni, lakini maamuzi yangu yalikuwa mepesi sana, ningekuta mvutano huo bado unaendelea na hakuna maamuzi ninegemuomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuichukua hiyo pesa na kuwaingizia watu wengine wenye uhitaji nazo, nitoe rai hizi pesa sio za kuchezea wala msitie pua zenu ni za moto, hakikihseni zinatumika kwa malengo kusudiwa na si vinginevyo" Amesema RC Sanare.
Hata hivyo ametoa agizo katika ujenzi huo wahakikishe wana simamia matumizi sahihi ya fedha kwa kufuata sheria pamoja na kuonesha thamani ya fedha katika miradi hiyo.
Kuhusu suala la mipaka, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba, kusimamia katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa mipaka ulipo baina ya Kata ya Magadu na Mbuyuni juu ya nani ni mmiliki halali wa Shule ya Sekondari SUA.
"Hakuna sababu ya kugombania mipaka, kikubwa baada ya suluhisho hilo kutatuliwa, wale ambao hawatakuwa na Shule waanzishe shule yao lakini nyie mtakaobakia na shule mtumie uungwana na upendo msaidiane katika ujenzi huo kwakuwa wote mlishiriki katika shule moja, mwenzko akijenga darasa moja na wewe unamsaidia moja, " Ameongeza RC Sanare.
Amesema changamoto ya baadhi ya Kata kutokuwa na Shule zinachangiwa na uzembe wa Watendajia au kukosekana kwa ardhi katika eneo husika.
Mwisho amewataka Watendaji kuacha kuvutana suala la mipaka badala yake wajikite katika ujenzi wa madarasa na Jengo la Utawala ili wanafunzi wasome kwa kuachiana nafasi baada ya hapo suala la mipaka litatafutiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema katika kukomesha migogoro ya namna hiyo pesa zitakazokuja katika bajeti ijayo zitakuwa zinaingizwa moja kwa moja katika akaunti za Shule badala za Kata ili kuepusha migogoro ya namna hiyo.
"Nimechukizwa sana na huu mgogoro, ni kweli Shule hii inasomeka ipo Kata ya Mbuyuni kabla ya Idara ya Elimu Msingi kurekebisha taarifa TAMISEMI,nilitoa agizo kwa Afisa Elimu Msingi juu ya kurekebisha taarifa ya Shule hiyo na sasa inasomeka ipo Kata ya Magadu , hata hivyo sisi hatukuangalia sana mipaka tulichokuwa tunataka ni Ujenzi wa Madarasa na Jengo la Utawala vikamilike ili waalimu na wanafunzi wawe katika mazingira mazuri ili watoto watakapofungua shule tuweze kupunguza msongamano darasani lakini kukaonekana kuna mvutano kati ya Diwani wa Kata ya Magadu na Mbuyuni hadi Mkuu wa Mkoa anaingilia kati na kutaka pesa hiyo itumike kwa namna yoyote , niwaombe hizi pesa ni kodi za wananchi hivyo tunavyozitoa zitumike kwa wakati na kwa malengo yaliyokusudiwa na zioneshe thamani ya pesa " Amesema Lukuba.
Naye Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu, amesema takribani milioni 39 zimetolewa ambapo shilingi milioni 14,500,000 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa pamoja na ununuzi wa madawati 80 na shilingi milioni 23 zitatumika kwa ajili ya Ujenzi wa Jengo la Utawala Ofisi ya Walaimu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa