Registration Insolvency & Trusteeship Agency(RITA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imesogeza huduma ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano ngazi ya kata na vituo vya kutoa huduma za Afya.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro Dr.Ikaji Rashid kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya kusajili na kutoa Vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa miaka mitano kwa wasajili wasaidizi.
Katika mafunzo hayo ambayo yamezinduliwa Desemba 4, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Morogoro,Dk. Ikaji, amesema vyeti hivyo vinatolewa bila malipo katika ngazi ya kata na vituo vya huduma za Afya kuanzia tarehe 6-17/12/2019, hivyo hatarajii kusikia Mwananchi yeyote atakayefika ngazi za Kata na vituo vya Tiba kutozwa fedha yoyote kwa ajili ya kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto.
Amesema kupitia mpango huo , kila kituo cha uandikishaji kitapewa simu kwa ajili ya kutuma taarifa za watoto watakaosajiliwa na wananchi watapaswa kufika katika vituo hivyo wakiwa na kadi ya kliniki ya mtoto na tangazo la uzazi,.
“Hakikisheni mnazitunza simu hizi na kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa si kwa matumizi mengine, pia huduma hii ni bure kwa yeyote atakayekiuka utaratibu huu, hatua kazi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na huduma hii itatolewa kwenye vituo tiba vinavyotoa huduma za baba, mama na mtoto hivyo haitakuwa na sababu mtoto kutokuwa na cheti cha kuzaliwa” Amesema Dr Ikaji
Dr Ikaji amesema kuwa kuanzishwa kwa mpango huo kutasaidia kuwaletea Wananchi huduma hiyo, huku akitoa rai huduma hiyo isitumike vibaya kama fursa ya kujipatia kipato kwa wale wote ambao Serikali imewapa dhamana ya kutoa huduma hiyo kwa ngazi ya Kata na Vituo vya Tiba.
Aidha, amesema Mafunzo hayo ni muhimu sana ambayo yataleta suluhisho kwa changamoto zilizokuwa zinasababisha watoto wengi kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa .
Amesema mojawapo ya changamoto kubwa ilikuwa ni umbali mrefu kutoka makazi ya Wananchi kabla ya kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambayo ilikuwa inahusika na utoaji wa Vyeti vya kuzaliwa.
Katika hatua nyengine, amechukua nafasi ya kutoa shukrani kwa RITA ambao wanasimamia mpango huo huku akiamini kuwa mpango huo ukitekelezwa kwa ufanisi, utaleta matokeo chanya katika utambuzi wa watoto.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa