RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuona ni namna gani ya kuwaruhusu wafanyabiashara wadogo (machinga) kuweza kuuza bidhaa zao ndani ya Kituo cha mabasi Msamvu kilichopo Manispaa ya Morogoro.
Rais Magufuli aliyasema hayo Jana wakati akifungua Kituo cha kisasa cha mabasi cha Msamvu kilichopo mjini hapa ambapo mradi wa ujenzi umegharimu kiasi cha shil. Bil.12.055 na kusimamiwa na kampuni ya ujenzi ya Group Six kwa kushirikiana kwa ubia kati ya LAPF na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Dkt Magufuli alisema kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha inajenga vituo mbalimbali vya kisasa vya mabasi ili wananchi waweze kuuza bidhaa zao na kuweza kunufaika na vituo hivyo.
Akitolea mfano wafanyabiashara ndogo ndogo Mkoani Morogoro kudai kuzuiwa kufanya shughuli zao za kuuuza bidhaa zao ndani ya Kituo hicho ikiwemo Chakula na Matunda kwa wasafiri alisema kuwa kitendo cha kuwazuia ni kuwanyanyasa wananchi hivyo Manispaa inapaswa kuwawekea mkakati wa kuwapa vitambulisho ili waweze Ku endelea kuuza bidhaa zao bila kubughudhiwa na mtu yoyote.
"Msiwazuie wamachinga kuuza bidhaa zao bali muwawekee mfumo mzuri kwani naamini hata mkiwaambia wachangie hata hela ya usafi watafanya hivyo" Alisema Rais Magufuli.
"Naagiza hivyo kwani lengo la serikali ni kuboresha maisha ya wananchi wake na sio kuwabagua na tunataka kuona Mkoa wa Morogoro unakuwa wa kisasa na wananchi kuweza kunufaika na fursa zilizopo na zinazozunguka mikoa jirani ikiwemo Dodoma na Dar es salaam. Alisema Rais Magufuli.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Msamvu Properties Company Eliudi Sanga akisoma taarifa za mradi wa ujenzi wa Kituo cha mabasi Msamvu alisema kuwa wazo la ujenzi wa kituo hicho cha kisasa ulianza mwaka 2008 baada ya kuona Kituo kilichokuwepo kuwa na mapungufu mengi na hakikuwa kinakusanya mapato ya kuridhisha.
Sanga alisema kuwa baada ya majadiliano ya kina mwaka 2009 Mfumo wa LAPF uliweza kutoa saini na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuanzia ujenzi wa Kituo cha mabasi cha kisasa eneo la Msamvu na kukiendesha kwa mfumo wa Kampuni.
Aidha Alisema kuwa kabla ya Kampuni hiyo kuanzishwa mapato yalikuwa ni wastani wa shil 350,000 kwa siku lakini baada ya Kampuni kuanza kusimamia hivi sasa mapato yameweza kuongezeka na kufikia shil Mil 3 kwa siku.
" Kutokana na ongezeko hilo tunatarajia kukusanya shil Bil.3.11 katika mwaka wa fedha 2017-2018 ikilinganishwa na shilingi Milioni 515. 5 zilizokusanywa mwaka 2013 .Alisema Sanga
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo wa Jimbo la Morogoro mjini (CCM) Abdulaziz Abood aliiweka wazi mbele ya rais Magufuli kuhusu ubadhiribu Mkubwa uliofanyika katika miradi ya mjini Morogoro.
"Mheshimiwa Rais kuna miradi mingi ya maji imefanyiwa ubadhirifu fedha mfano mradi wa maji wa Kipera uliotumia shil Mil 500,mradi wa Kiegea,Kasanga,Mkorea, ambapo jumla ya Bili.1.56 zimeteketea na hivyo wananchi kukosa Huduma ya Maji safi Na salama" Alisema Abood.
Abood alisema kutokana na changamoto hiyo ya miradi kuonekana fedha zake zimeteketea na kushindwa kumletea tija mwananchi amemuomba Rais Magufuli aingilie kati ambapo sanjari na hayo Rais amemuagiza Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jaffo kufanya uchunguzi Juu ya ubadhirifu huo.
Hata hivyo Kituo cha mabasi cha Msamvu ni miongoni mwa kituo Vya kisasa vlivyojengwa nchini ambapo kinatoa Huduma mbalimbalimbali ikiwemo mfumo WA usalama (CCT kamera,mgahawa Mkubwa wa Chakula,sehemu ya kusubiria abiria,mabenki,vibanda Vya biashara ,jengo la utawala nk.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa