Idadi ya wanawake wajawazito wanaojifungulia katika Vituo vya huduma Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeongezeka kutoka asilimia 97 kwa mwaka 2017/ 2018 hadi kufikia asilimia 99 mwaka 2018/2019.
Licha ya ongezeko hilo , vituo vya Afya vinavyotoa huduma ya kupima wingi wa damu kwa akina mama wajawazito vimeongezeka kutoka vituo vitatu mwaka 2017/2018 na kufikia 19 kwa mwaka 2018/2019.
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga alisema hayo katika mkutano wa kawaida wa mwaka wa Baraza la Madiwani ambao ulioambatana na uchangzi wa nafasi ya Naibu Meya pamoja na wenyeviti wa kamati ya Mipangomiji na Mazingira, Kamati ya Maadili ya Madiwani na Kamati ya huduma za jamii.
Kihanga alisema ,Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani , Watendaji na wananchi imefanikisha kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za uchumi na uwekezaji ,miundombinu , ardhi, elimu ya msingi na sekondari, mazingira ,maji , kilimo, utawala bora , afya na nyinginezo.
Kwa upande wa sekta ya afya alisema,kumekuwepo na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka kituo kimoja hadi kufikia viwili mwaka 2018/2019.
Alisema ,Halmashauri pia imeweza kununua mashine mbili za Ultrasound na kuziweka katika vituo vya Afya Mafiga na Kingolwira pamoja na ukarabati wa Kituo cha Afya Kingolwira unaoendelea sambamba na ujenzi wa wodi ya wazazi kwenye Kituo cha Afya Saba Saba.
Kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) Meya alisema ,Halmashauri ina jumla ya walengwa 2,850 hadi kufikia Juni , 2019 wanaishi katika mitaa 164 kutoka kwenye kata zote 29 ambao wamenufaika kwa jumla ya Sh milioni 378.5 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Hata hivyo alisema , jumla ya kaya 874 za wa TASAF III wameweza kujiwekea akiba kwa ajili ya kuhudumia matibabu ya familia zao kwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa baada ya kuhamasishaji.
Wakati huo huo , Baraza la Madiwani lilimchagua kwa mara nyingine tena Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege , Isihaka Sengo (CCM) kuwa Naibu Meya baada ya kupata kura 34 na kumshinda Diwani wa Viti Maalumu, Scolastika Mkude ( Chadema ) aliyepata kura tano ambazo ni za madiwani wa Chama hicho.
Mkurugenzi wa Manispaa John Mgalula pia aliwatangaza wenyeviti wa kamati za baraza waliochanguliwa na madiwani wenzao wote kutoka CCM ni Spear Komanya mwenyekiti wa kamati ya huduma ya jamii , Ally Kalungwana mwenyekiti wa kamati ya Mipangomiji na Mazingira , na Madaraka Byanguze mwenyekiti wa kamati ya maadili ya Madiwani wakati Naibu Meya akiingia moja kwa moja kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa