Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesema inaangalia ni lipi la kufanya ili kuhakikisha awamu ya pili ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuendela na ukarabati wa maeneo mengine ya shule kongwe nchini ambazo hazijafikiwa ziweze kutumika ipasavyo kulingana na ubora wa thamani halisi ya fedha zilizotumika.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati akizungumza na uongozi wa mkoa wa Morogoro , wilaya ya Morogoro pamoja na uongozi wa shule ya sekondari Kilakala iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kimkakati inayotekelezwa na serikali katika maeneo ya mikoa mbalimbali nchini ukiwemo wa Morogoro katika soko kuu na shule ya Sekondari Kilakala pamoja na Mzumbe kwa lengo la kuangalia thamani halisi ya fedha zilizotumika.
“ Nimekuja kuona ukarabati uliofanyika hapa Sekondari ya Kilakala yakiwemo Mabweni manane yamekarabatiwa kwa fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya tano kiasi cha Sh milioni 935.5 kupitia Mamkala ya Elimu Tanzania (TEA) na kazi hii ya ukarabati imefanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alisema Dk Kijaji.
Naibu Waziri aliongeza kusema “ Baada ya taarifa ya awali ya ukaguzi , nimekuja kuona hali halisi , lakini yapo mapungufu katika ukarabati wa shule hii , baadhi ya maeneo ukarabati haujafanyika vizuri hivyo wahusika wanapaswa kuja kurekebisha mapungufu haya “ alisema Dk Kijaji.
Hata hivyo alisema Wizara inayohusika na upelekaji wa fedha itakaa na Serikali ili kujua lipi la kufanya ili kuhakikisha awamu ya pili ya fedha zinazokuja kwa ajili ya kuendelea na ukarabati maeneo mengine ambayo hajayafikiwa ziweze kutumika ipasavyo.
Katika taarifa ya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya shule hiyo kongwe ,Uongozi wa Shule ya Sekondari Kilakala, umeipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kazi nzuri ya kukarabati shule zake kongwe nchini ikiwemo shule yao ambayo awamu ya kwanza ilitengewa kiasi cha Sh milioni 935.5.
Mkuu wa Shule hiyo ya wasichana ya vipaji maalumu ( Ufaulu wa juu), Mildreda Selula alisema kuwa , katika ukarabati wa miundombinu ya majengo ya shule hiyo awamu ya kwanza ulihusisha mabweni 13, madarasa nane , maabara sita , ofisi kuu , bwalo la chakula , sehemu ya kufulia nguo pamoja na miundombinu ya umeme na maji.
Hata hvyo alisema , kazi hiyo iliyofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) chini ya ufadhili wa Mamkala ya Elimu Tanzania (TEA) licha ya kukamilika kwake , bado kuna mapungufu kadhaa yaliyoainishiwa na timu ya wataalamu wa kutoka Ofisi ya Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro yakiwemo kabati zilizotolewa mabwenini hazikurudishiwa .
“ Ukarabati ulifanyika vizuri na mazingira ya shule yetu yanapendeza , kazi hii kwa awamu ya kwanza imekamilika japokuwa kuna mapungufu kadhaa yaliyobainishwa na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro” alisema Selula.
Mkuu wa Shule hiyo alitaja mapungufu hayo ni baadhi ya mabweni madirisha yake hayakuwekwa nyavu za kuzuia mbu na aliyataja kuwa ni Ruhinda, Kimweri, Ntara na Rugambwa , pia milango ya vyumba vya stoo mabwenini haikurudishiwa kama ilivyokuwa awali.
Selula alitaja mapungufu mengine ni rangi iliyopakwa katika majengo haikua katika ubora unaotakiwa na baadhi ya mabweni sakafu iliyowekwa si imara kwani zina nyufa.
Pamoja na hayo alisema kuwa, baadhi ya vyumba vya maabara vioo vya ‘ruvas’ hazikuwekwa kama ilivyo awali, mifumo ya maabara na fenicha ( sofa) hazikukarabatiwa , dari ( Gypsum ) katika majengo yote ya mabweni haikuwekwa kama ilivyotakiwa na swichi kuu za umeme zilizopo hazina ubora unaotakiwa.
Mkuu wa Shule hiyo alisema , uongozi wa shule unaanimi kuwa ukarabati utakapomalizika kwa awamu zote tatu mazingira ya kujifunzia na kufundishia yataboreka na ufaulu utaongezeka .
Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo , na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga kwa nyakati tofauti walisema mbele ya Naibu Waziri huyo kuwa TEA ilitoa zabuni kwa Shirika la NHC na kwamba uongozi wa wilaya na Halmashauri haukuweza kuuona mkataba wake ingawa walielekeza kuwa mapungufu yaliyojitokeza wayarekebishe .
“ Shule hizi kongwe ndizo ni kioo cha jamii kwani zinachukua wanafunzi wa mikoa mbalimbali hapa nchini , hivyo ni vyema Serikali iziangalie kwa ukaribu zaidi” alisema Meya Kihanga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa