DIWANI wa Kata ya Luhungo, Mhe. Abdallah Chamgulu, amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma kwa Wazee hususani Wazee wa Kata ya Luhungo.
Kauli hiyo ameisema Oktoba 21/2021 katika sherehe za uzinduzi wa Baraza la Wazee Kata ya Luhungo pamoja na kuwasimika Viongozi wa Wazee kuanzia ngazi za Mitaa na Kata.
Akizungumza na Wazee waliojitokeza katika uzinduzi huo wa Baraza la kuwasimika Viongozi, Mhe. Chamgulu , amesema kuwa Serikali inatambua kuwa wazee ni hazina katika kuibua na kuchochea shughuli mbalimbali za kimaendeleo kutokana na ushauri mzuri wanaotoa wanaposhirikishwa katika mambo ya kimaendeleo.
"Serikali itaendelea kujiimarisha katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa Wazee kwa kuzingatia umuhimu wa kundi hili katika jamii yetu , Manispaa yetu ya Morogoro kwa kuwatambua Wazee wameanza kutatua changamoto ya vitambulisho vya msamaha wa matibabu bure kwa wazee wetu , hii ni hatua kubwa ambayo Manispaa yetu imeifanya na sio mwisho hapa Luhungo kuna Mitaa 7 lakini Mitaa 4 ndio wazee wamepata vitambulisho na hiyo iliyobakia katika zoezi lijalo basi tutaipunguza na kufanya Mitaa yote 7 inafikiwa na huduma hii"Amesema Mhe. Chamgulu.
Aidha, Chamgulu, amesema kwa Mitaa ambayo haijafikiwa na huduma hiyo ya vitambulisho, Ofisi ya Kata imeandaa utaratibu mzuri wa kuwaandikia barua za kuwatambua wazee hao ili na wao waendelee kupatiwa huduma kama wengine huku wakiendelea na wao kupatiwa vitambulisho vyao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chamgulu, amesema Serikali itahakikisha kwamba wanaenda kutatua changamoto za haraka kwa Wazee kupata stahiki zao mapema pindi wanapo staafu kazi ili waweze kujikimu wakiwa nyumbani.
Naye, Mratibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Rehema Malimi, amesema katika kuona Baraza hilo la Wazee linatimiza majukumu yake vizuri wataandaa semina kwa viongozi wao ili kila mmoja kujua majukumu yake na mipaka yao katika kuwatumikia wazee.
Malimi, amewahimiza wazee kuwa na utaratibu wa kwenda kucheki afya zao mara kwa mara ili kupata huduma stahiki kwa wakati kwani huduma za afya kwa wazee kuanzia miaka 60 ni bure katika vituo vyote vya kutolea huduma.
Kupitia Uzinduzi huo wa Baraza na kuwasimika Viongozi, Bi. Malimi, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazee hao juu ya UVIKO-19 na kuwataka wazee kuendelea kuchanja, kwani wapo kwenye kundi ambalo ni rahisi kupata maambukizi hayo huku akiwatoa hofu kwamba chanjo hii ni salama kabisa na kuwataka kumuunga mkono Mhe.Rais alieona umuhimu wa kuokoa maisha ya watanzania kwa kupata chanjo hii.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro, Mzee Samweli Mpeka, amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee ikiwa ni pamoja upungufu wa dawa na wataalam wa kuhudumia wazee,umaskini uliokithiri kutokana na kipato duni au kutokuwa na kipato kabisa sambamba na wazee kutokupewa kipaumbele kama makundi mengine kama vile wanawake,vijana na walemavu.
Halmashauri ya manispaa ya Morogoro imeungana na Kata ya Luhungo , katika sherehe za Uzinduzi wa Baraza la Wazee Kata ya Luhungo pamoja na kuwasimika Viongozi wa Mabaraza hayo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa