Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini , Abdulaziz Abood,amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa ,serikali ya awamu ya tano imejipanga kumaliza changamoto zote zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa huduma bora ya maji safi na salama .
Mpango huo ukiwa ni pamoja na kujengwa kwa soko la kisasa na kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya wilaya itakayowezesha kupatikana kwa huduma za kisasa cha tiba kwa wananchi.
Abood alisema hayo juzi wakati wa ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika Kata ya Mwembesongo , Mazimbu na Mji mpya zilizopo Manispaa ambapo pia alichangia fedha na vifaa vya kumalizia miradi iliyopo katika kata hizo.
Alisema, siku zote kitu ambacho alikuwa akikipigania kwa nguvu zote anapokuwa Bungeni ni kuhusu tatizo la maji katika Manispaa ya Morogoro ambapo sasa Serikali imetambua jambo hilo na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji.
“ Binafsi nikiwa bungeni nimebatizwa jina la bwana maji, maana kila nikisimama nazungumzia maji, kwakuwa ninajua tatizo kubwa kwa wananchi wangu ndio hilo” alisema Abood na kuongeza kwa kusema .
“ Nashukuru sasa tayari serikali imeshanielewa , na tumepata mradi mkubwa wa maji na tayari mkandarasi ameshasaini kuanza kazi mara moja na muda si mrefu tutaondokana na tatizo hili” alisema Abood.
Kuhusu hospitali ya wilaya alisema, amewasiliana na Waziri wa TAMISEMI na amehamikishia kuwa zitatolewa fedha kwa ajili ujenzi wa wodi ya kisasa, chumba cha upasuaji na nyumba ya mganga ili iweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa kata zilizopo pembezoni mwa Manispaa .
Mbunge huyo alisema , licha ya kuchangia ujenzi wa zahanati kila kata ,amewalipia bima ya afya (CHF iliyoboreshwa ) wazee wote kila kata ili kupata huduma za matibabu katika zahanati na vituo vya afya.
Kuhusu sekta ya elimu alisema , ametoa mifuko 100 ya saruji na nondo kwa kila darasa linalojengwa kila kata ili kumaliza changamoto ya upungufu wa madarasa.
Kwa upande wa Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga ambaye ni Diwani wa kata ya Mazimbu alisema, kupitia Mbunge huyo shughuli za kimaendeleo zimefanyika na kukamilishwa ikiwemo kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa , kujengwa barabara za kiwango cha lami na kuiwezesha Manispaa kuwa na sifa ya kuelekea kuwa Jiji.
Hivyo alisema , katika kuboresha huduma za usafiri tayari Manispaa inatarajia kujenga stendi ndogo ya kisasa ya mabasi yanayofanya safari ndani ya Manispaa pamoja na eneo la maegesho ya magari makubwa ya mizigo.
Naye Ofisa Mtendaji wa kata ya Mazimbu, Alatutosia Sanga alimshukuru mbunge kwa kutoa Sh milioni sita kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa mazingira mto Ngerengere ambao ulikuwa ukimwaga maji kwenye makazi ya wananchi wa Mazimbu na ujenzi wa zahanati , vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Mazimbu A na B.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa