Wanafunzi wa shule ya Msingi Uhuru iliyopo Manispaa ya Morogoro wametakiwa kujenga tabia ya kusoma vitabu ili kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali ya kisanyansi na kijamii ili kupata maarifa na kujiwekea mazingira mazuri ya ufaulu wa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Muasisi na Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Dr Ntuyabaliwe Foundation ,Jacqueline Mengi alisema hayo hivi karibuni mara baada ya kuzindua maktaba yenye vitabu vya kitaaluma na hadhithi alivyokabidhi kwa uongozi wa shule ya msingi Uhuru kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kujisomea nyakati za masomo shuleni hapo.
Alisema ,lengo la Taasisi ya Dr Ntuyabaliwe Foundation ni kuhimiza watoto hususani wanafunzi kupenda kujisomea vitabu ili kujenga maarifa na msingi wa maisha katika siku za usoni.
“Taasisi inazindua maktaba ya shule ya Msingi Uhuru ya Manispaa ya Morogoro na inawahusu wanafunzi wote ili wasome vitabu kwa ajili yakujenga uelewa na wasisome kwa ajili ya kufauli mtihani bali kila siku “ alisema Mama Mengi.
Muasisi na Mkurugenzi mkuu huyo alisema ,tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Dr Ntuyabaliwe Foundation ,hiyo ni mara ya kwanza kuweza kufungua maktaba ya vitabu kwa shule ya msingi nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema ,Taasisi hiyo ina unga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika masuala ya uboreshaji wa elimu na kwa kufanya hivyo imeweka mpango endelevu wa kufungua maktaba za vitabu kwa shule za msingi nje ya mkoa huo wa Dar es Salaam.
“ Nimefurahi kuona tumeanza kupiga hatua kubwa , lengo la Taasisi ni kufungua maktaba za vitabu kila mkoa nchini na ikiwezekana hadi ngazi ya kila wilaya ili kila shule inakuwa na maktaba iliyoanzishwa na Taasisi ya Dr Ntuyabaliwe “ alisema mke wa Mengi .
Naye Mkuu wa shule ya Msingi Uhuru iliyopo Kata ya Uwanja wa Taifa,Manispaa ya Morogoro, Muchunguzi Lutagwelera , alimpongeza mama Mengi na Taasisi yake kwa kuona umuhimu wa kuisaidia shule hiyo kukarabati chumba cha darasa na kufungua maktaba ya vitabu kwa ajili ya kujisomea wanafunzi na kuwawezesha kuongeza kiwango cha ufaulu.
Alisema , shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1971 hadi sasa ina wanafunzi 1,651 kati hayo wavulana 844 na wasichana 807 na licha ya changamoto kadhaa imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya darasa la nne na la saba kuwa katika kumi bora kwenye shule za msingi za Manispaa ya Morogoro.
Nao wanafunzi wa shule hiyo katika risala yao kwa mgeni rasmi iliyosomwa na dada wa shule , Regina Julias pamoja na kutoa shukrani nyingi kwa Taasisi ya Dr Ntuyabaliwe Foundatin kwa kuweza kuichagua shule yao kuiwezesha kuwa na chumba cha Maktaba.
“ Tunaahidi tunaitunza maktaba hii pamoja na vifaa vyote vilivyomo ili viweze kudumu na kusaidia wanafunzo wote hata wale ambao hawajaanza shule “ alisema Regina.
Hata hivyo walimwomba awe mlezi wa shule hiyo na kushirikiana na uongozi wa shule katika kuondoa kero kubwa ya uzio , madarasa , matundu ya vyoo na samani .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa