Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro ,imezindua warsha ya wadau wa Elimu kujadili matokeo ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za ruzuku kwa ajili ya Shule za Msingi (Capitation Grant).
Warsha hiyo ya wadau wa Elimu kujadili matokeo ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Ruzuku kwa ajili ya Shule za Msingi (Capitation Grant) imefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Novemba 14, 2019 .
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Warsha hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Eng. Emmanuel Kalobelo, ameipongeza TAKUKURU kwa kuandaa mafunzo hayo ya kujadili matokeo ya ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo na ruzuku mashuleni, kwani yatasaidia kupunguza mlundikano wa kesi za matumizi mabaya ya pesa za ruzuku katika Shule zinazoletwa kwa lengo maalumu kwa ajili ya kukuza elimu hapa nchini.
Aidha, amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Tano Chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imewekeza sana katika mpango wa elimu bila malipo, hivyo ni wajibu wa walimu kuzitumia pesa hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema TAKUKURU imefanya uchambuzi kwenye mfumo wa utawala wa fedha na ruzuku za uendeshaji kwa ajili ya shule za msingi ( Capitation Grant) ili kubaini changamoto zilizopo ambazo kwa maoni ya TAKUKURU ni kiini cha vitendo vya Rushwa na hatimaye kuishauri Serikali namna bora ya kuziba mianya hiyo.
Aidha amesema msukumo wa kufanya ufuatiliaji huo umetokana na mapungufu yanayolalamikiwa na wananchi kwenye matumizi ya fedha hizo,na kueleza mpango wa elimu bila malipo uliasisiwa vizuri kwa ajili ya kukuza elimu hapa nchini, hivyo pesa za ruzuku zinaletwa kwa lengo la ununuzi wa vifaa pamoja na kukarabati mazingira ya shule na majengo yake.
"Nawapongeza sana TAKUKURU, katika kufanya kazi hii naamini wengi wenu mmeshirikishwa kwa njia moja au nyingine kufanikisha kazi hii , hivyo nichukue nafasi hii kuwapongeza wote mlioshiriki kwa moyo wenu wa uzalendo, niwaombe waalimu jitahidini kupunguza malalamiko kwa wananchi dhidi ya tuhuma za matumizi mabaya ya ruzuku za pesa shuleni" Amesema Eng. Kalobelo.
Pia alieleza kuwa kumekuwepo na malalmiko mengi katika ofisi yake dhidi ya matumizi mabaya ya pesa za ruzuku shuleni, hivyo amewataka Waalimu malalamiko hayo yasikilizwe ngazi za chini kwani katika kila shule kuna kamati za shule na sio kuyaleta kwake labda pale wanapoona kuna kushindwa kufikia muafaka.
Amesema kuwa , kazi ya kufanya ufuatiliaji imekoma, hivyo TAKUKURU wamewakutanisha hapo kwa kutoa mirejesho, anaamini mirejesho hiyo itaendana na majukumu kwa kila mdau na utekelezaji utakuwa kwa kipindi maalumu, amewaomba wadau kuwa mapendekezo yaliyotolewa yawe kama sehemu ya suluhisho ya changamoto zilizojitokeza na zifanyiwe kazi kwa kasi na endapo kuna kukwama TAKUKURU watakuwepo kwa ajili ya ufafanuzi.
"" Sihitaji kuona malalamiko tena katika ofisi yangu,niwakumbushe kuwa tunawajibu wa kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko ya wananchi kwenye huduma za Serikali, naomba kuwakumbusha tena kuwa mwajiri wetu ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali inatokana na Wananchi, wenye Serikali ni Wananchi hivyo malalamiko ya Wananchi dhidi ya huduma ya Serikali kwenye maeneo yenu inaweza kutafsiriwa kwenye uzembe, utovu wa maadili na rushwa"" Ameongeza Eng. Kalobelo.
Amesema kuwa, kuna hatua mbali mbali zilizochukuliwa katika Mkoa wa Morogoro kwenye mapambano dhidi ya rushwa kwa kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Jemedari Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kipindi cha miaka minne, Mkoa wa Morogoro kwa maana ya Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Manispaa, Halmashauri ya Wilaya, Kata na Serikali ya Vijiji, vitongoji na Mitaa imetekeleza Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na mapango wa Utekelezaji Awamu ya tatu (2007-2022) tayari wameunda kamati za kudhibiti Uadilifu, wajumbe wa kamati za kudhibi Uadilifu na kamati za uongozi na uratibu zimewezeshwa na tayari taarifa za kila robo Mwaka zinawasilishwa kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Eng. Joyce Baravuga, amemshukuru Mhe. Rais Dkt John Magufuli kwa kuanzisha sera ya elimu bila malipo na kwamba Wananchi wengi wameweza kupata fursa kwa kuwaandikisha watoto wao shuleni.
Amesema Muongozo wa matumizi ya fedha za ruzuku za Serikali kwa Shule za Msingi unawahusika wapatao 11, miongoni mwao ni pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kazi yake ni kutoa sera na waraka, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye mamlaka ya kutoa vibali maalumu vya michango shuleni pale inapohitajika, Mkuu wa Wilaya ambaye atakuwa msimaizi wa uvunjifu wa sheria shuleni, Wakurugenzi wa Halmsahauri na Manispaa ambao kazi yao ni kutoa mipango ya bajeti kwa TAMISEMI ili ruzuku zifike shuleni, Maafisa Elimu, Kamati za Shule, Waalimu, Wanafunzi, Mzazi/mlezi pamoja na Jamii inayowazungukla.
Aidha amesema mpaka sasa Mkoa wa Morogoro una jumla ya Waalimu 9466 wa Shule za Msingi, Wanafunzi laki 529412 pamoja na shule za Msingi 910.
Amesema kwa mwaka kila mwanafunzi anatakiwa kupokea shilingi 10000/=, ambapo kuanzia mwezi Juni 2018 hadi Julai 2019 pesa zilizoingizwa ni shilingi Bilioni 2.2 kwa shule za msingi.
Pia amesema vipaumbele 5 vimemeweka katika muongozo wa fedha za ruzuku za mpango wa elimu bila malipo, miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kununulia vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa 30%, ukarabati wa shule kwa 30%, uendeshaji wa mitihani shuleni shule kwa 20%, kuendesha michezo 10% pamoja na utawala kwa 10%.
Kwa upande wa Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Morogoro Abdul Buhety, ameipongeza TAKUKURU kwa kuandaa warsha hiyo, huku akisema kuanzia Desemba 2015, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa shule za msingi wamekuwa wakipokea fedha za ruzuku takribani Shilingi Milioni 26 na laki mbili kwa kila mwezi, japo kuna changamoto zinazojitokeza licha ya kuwepo kwa ruzuku ya fedha shuleni kwa elimu bila malipo.
Amezitaja changamoto hizo, ambapo miongoni mwa changamoto ni pamoja na kuongezeka kwa uhaba wa miundombinu , kusua sua kwa ukarabati wa shule, Kiasi cha fedha kinachopelekwa shuleni hakitoshelezi kwani wana mahitaji kama vile, Maji, Umeme pamoja na Chakula kwa Wanafunzi.
Pia ameiomba Serikali ibadili viwango vya pesa ya mwanafunzi kwa mwaka , kwani kiasi cha Shilingi 10000/= kwa mwaka ni kiwango kilichopitwa na wakati kutokana na shule kukabiliwa na changamoto nyingi.
“Niwaombe Wadau wa elimu endeleeni kutoa elimu kwa Wazazi juu ya elimu bila malipo ikiwamo kuwasisitizia wazazi kuwasaidia watoto zao kuwanunulia vitu kama vile Nguo za shule( Uniform) pamoja na vitendea kazi madaftari na mabegi” Amesema Afisa Elimu msingi
Ameiomba Serikali asilimia 10% ya fedha ya michezo ikatwe moja kwa moja kutoka hadhina kwenda kwenye akaunti za Shule ili ziweze kutumika kwa wakati na kuboresha michezo Shuleni.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa