Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amewaasa watumishi wa Wilaya ya Morogoro kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 22/2021 wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Ndg. Bakari Msulwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo ya Ofisi, DC Msando, amewataka watumishi kutoa ushirikiano wa dhati na kuwa na ari ya kufanya kazi ili waweze kufanikiwa zaidi huku akiwataka watumishi hao kutokukasirika pindi watakapohimizwa kutekeleza majukumu yao.
"Napenda kusema kuwa kama tutaendelea na ushirikiano huu naamini Wilaya yetu itakuwa salama , naamini kwa dhati kuwa kaka yangu Bakari Msulwa ,amefanya kazi kubwa sana na mimi pale alipoishia nitaendeleza , tunashukuru sana kaka yetu Msulwa uliyekuwa chachu ya mabadiliko ndani ya Wilaya ya Morogoro na watumishi hawa wamejifunza mengi kutoka kwako, mimi niwatoe wasiwasi watumishi nitatoa ushirikiano kwenu nanyi mnipe ushirikiano ili tuipeleke wilaya yetu mbele" Amesema DC Msando.
Aidha, amewataka watumishi kufanya kazi kwa mshikamano na kuepuka majungu yasiyo na tija na kuweka chuki ambazo zinaharibu taswira ya Wilaya na Viongozi kwa ujumla.
"Mimi nataka kazi kwanza majungu sipendi, Ofisi yangu ipo wazi masaa 24, una jambo njoo tuzungumze na kama una chakushauri njoo na tusifichane taarifa maana tukizikumbatia hizi taarifa mwishoni zinaweza kutuingiza matatani, ukiona nakuita nje ya muda wa kazi naomba sana uzingatie wito lengo sio kukomoana bali tunataka kujenga Wilaya yetu na kuweza kuwatumikia wananchi kwa kutoa huduma bora" Ameongeza DC Msando.
Mwisho, amewashukuru sana watumishi pamoja na wananchi kwa kuonesha ukarimu mkubwa wa kumpokea huku akiamini kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kuweza kushirikiana .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa