Mkuu wa mkoa Morogoro Dk Kebwe Stephen Kebwe ameiagiza Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Nandhra inayojenga Soko Kuu la Morogoro kufanya kazi usiku na mchana ili kufidia muda ambao wataweza kuupoteza wakati wa mvua za masika zitakapoanza ili ujenzi huo ukamilike katika muda ulipangwa wa Septemba 19, mwaka huu.
Dk Kebwe alitoa agizo hilo alipofanya ziara katika soko hilo Jan 2, 2019 ili kuona shughuli za ujenzi akiambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kwa lengo la kubaini kama kuna changamoto na mapungufu yoyote.
Hata hivyo baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo. mkuu wa mkoa alibaini ujenzi uko nyuma ya ratiba ya kukamilika kwake kwa wiki tano na kuamua kufikia hatua ya kuagiza ujenzi huo kufanyika usiku na mchana.
“Mradi uko nyuma ya ratiba ya kukamilika kwake na ili kwenda na muda uliowekwa katika mkataba mkandarasi nakuelekeza jengeni usiku na mchana ili hata kama ikitokea bahati mbaya mvua zitakuja kwa wingi muwe tayari mmekwisha okoa sehemu ya muda” alisema Dk Kebwe.
Hata hivyo Mkuu wa mkoa alimshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kuweza kutoa fedha hizo kwani halmashauri yenyewe isingekuwa na uwezo wa kuwa na fedha za kujenga soko la kisasa la Morogoro.
Naye Meya wa Manispaa ya Morogoro aliwatoa hofu wafanyabiashara kuwa, wataendelea kutekeleza makubaliano waliyokubaliana awali kwa wafanyabiashara waliokuwa soko la zamani kabla ya kuvunjwa kupisha ujenzi huo watakuwa wa kwanza kupewa vizimba vya kufanyia biashara zao.
“ Ujenzi wa soko hili utakapokamilika kipaumbele kitawekwa kwa wafanyabiashara waliopisha ujenzi wapo zaidi ya 1,000 ambao tumewapeleka kwa muda soko la Manzese na litaluwa na eneo la wafanyabiashara wa mboga na litakuwa na vibanda vingi vya maduka zaidi ya 160 na maeneo ya kutolea huduma mbalimbali za kijamii” alisema Kihanga.
Hata hivyo kwa niaba ya wananchi wa Manispaa hiyo. alimshukuru Rais na kusema kuwa ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa miradi endelevu itakayoiingizia halmashauri mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake msimamizi wa Ujenzi wa soko hilo, Mhandisi Antonio Mkinga alitaja changamoto za mradi ikiwa ni pamoja na eneo la mradi liko chini sana na kuwepo kwa mto Kikundi unaopita karibu na eneo hilo na kuweza kuathiri kwa kiasi mwenendo wa ujenzi , huku Meneja wa mradi huo kutoka Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Nandhra , Rabinder Singh aliwahakishia mkuu wa mkoa kuwa wataanza kujenga usiku na mchana.
Soko hilo kubwa la kisasa lenye ghorofa moja linajengwa baada ya Wizara ya fedha kupitia Hazina kupatia halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sh bilioni 17.6 baada ya soko la zamani iliyojengwa mwaka 1953 kuvunjwa na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 15 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 19 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa