Tatizo la wanawake wajawazito kujifungua kumulikiwa taa ya kandili na kurunzi za simu katika Zahanati ya Towelo ,iliyopo Manispaa ya Morogoro litabaki historia mara baada ya Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), mkoa wa Morogoro kupeleka umeme ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri wa Nishati .
Naibu Waziri wa Nishati , Subira Mgalu , machi mwaka huu aliitembelea Zahanati hiyo iliyojengwa katika safu ya milima ya Ulunguru ambapo alijionea haina umeme na kutoa agizo hilo kwa Shirika hilo kufikishia umeme .
Katika ziara hiyo viongozi mtaa wa Towelo na wananchi waliwasilisha malalamiko kwa Naibu Waziri juu ya changamoto wanazozipata hasa wanawake wajawazito kumulikiwa na taa za kandiri na kurunzi za simu wakati wa kujifungua.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo hivi karibuni akiwa wilayani Morogoro aliitembelea tena Zahanati hiyo kwa ajili ya kuona utekelezaji wa agizo lake na alipofika alikuta umeme ukiwa unawaka.
Akiwa katika Zahanati hiyo , Naibu waziri aliwataka wauguzi na wakunga kuwahudumia wananchi kwa kukaa muda wa saa 24 katika Zahanati hiyo kwa vile kisingizio cha haina umeme sasa kimeondolewa .
Naye Mjumbe wa kamati ya zahanati hiyo, Siajabu Abeid akizungumza mbele ya Naibu Waziri mara baada ya kufikishwa kwa umeme katika Zahanati hiyo alisema, huduma za matibabu zinatolewa saa 24 tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo usiku ilikuwa ikifungwa .
Alisema, uwepo wa umeme katika Zahanati hiyo ,kumeondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili wagonjwa ya kukosa vipimo vinavyotumia umeme vikiwemo vya malaria.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri, Kaimu meneja wa Tanesco mkoa wa Morogoro Mhandisi Lawrence Maro alisema, upelekaji umeme katika Zahanati hiyo umegharimu zaidi ya Sh. 54 milioni fedha ambazo zilitokana na vyanzo vya ndani.
Mhandisi Maro alisema, kutokana na ukubwa wa transfoma waliyoiweka wameweza pia kupeleka umeme huo katika shule ya msingi ya Towelo iliyopo katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine Naibu waziri huyo pia alizindua uwashaji umeme katika kijiji cha Mtego wa Simba kilichopo Kata ya Mkambalani , halmashauri ya Wilaya ya Morogoro utakaosambazwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alisema, katika bajeti iliyopitishwa hivi karibuni , mkoa wa Morogoro umetengewa kiasi cha Sh: Bilioni 45 kwa ajili ya kujenga miundombinu na kusambaza umeme kwenye vijiji 150 kupitia mradi wa Rea. .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa