Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mheshimiwa Rebecca Nsemwa, leo tarehe 29.01.2023 amepokea msaada wa chakula, sabuni, na mavazi kutoka kwa Kamati ya Maafa yaUmoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoa wa Morogoro, msaada uliolengakuwafariji wananchi wa Manispaa ya Morogoro, waliopatwa na maafa kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.
Mara baada ya kupokea msaada huo, mheshimiwa Nsemwa amewashukuru wananwake wa (UWT) mkoa wa Morogoro kwa tendo hilo jema walilofanya, kishaakatoa wito kwa watu mbalimbali, taasisi na mashirika yaliyomo ndani na nje ya Morogoro kujitokeza kuwasaidia wananchi walioathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwani msaada kama huo wa chakula na mavazi unahitajika sana kwao kwa sababu maafa ni jambo ambalo mtu hapangi limkute.
Mheshimiwa Nsemwa ametoa wito kwa wananchi ambao bado wanaishi kwenye maeneo ambayo ni mikondo ya maji, waondoke kwenye maeneo hayo kwani mvua bado zinaendelea kunyesha na huenda zikaunganisha na mvua za masika, hivyo ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuhama kwenye maeneo yote hatarishi.
Aidha, mheshimiwa Nsemwa amevipongeza vikosi vya uokoaji vya Wilaya kwa msaada mkubwa uliosaidia wananchi kuwa salama, walioutoa siku chache zilizopita baada ya maji kuathiri makazi ya watu na mali zao.
“Juzi vikosi vyetu vya uokoaji viligawana maeneo ya kufanya uokoaji na hii ilisaidia sana wananchi wetu kuwa salama. Lakini pia tunashukuru kwamba mvua ilinyesha mchana huenda ingenyesha usiku maafa yangekuwa makubwa zaidi. Ninawasihi wananchi katika kipindi hiki, punguzeni safari za usiku zisizokuwa za lazima, na mnapofikwa na majanga msipaniki bali kuweni watulivu na mpige simu Ofisini kwangu ili tuweze kuwapatia msaada wa uokozi kupitia vikosi vyetu vya uokoaji. Mkipaniki na kuanza kukimbia huku na kule mnaweza kusombwa na maji” alieleza Nsemwa.
Kwa upande wake Katibu wa UWT mkoa wa Morogoro, ndugu Mwajabu Ally Maguluku,ambaye ndiye alikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, amesema msaada walioutoa una thamani isiyo pungua shilingi laki tano za Tanzania, na kwamba imekuwa ni desturi yao kutoa misaada kama hiyo katika kipindi hiki ambapo awali, walifanya hivyo kwa maeneo ya Kilosa, Hanang, na Mvomero.
Amesema Wanawake wa UWT wataendelea kuchangishana ili kuendelea kuleta msaada kwa waathirika wa ndani ya Manispaa ya Morogoro. Lakini pia amemshukuru mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mheshimiwa Abood kwa kuwa tayari kuwapatia usafiri kila mara wanapohitaji kwenda mahali fulani kupeleka misaada kwa waathirika wa mvua.
Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), wametoa msaada huo ikiwa ni namna yaoya kuadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa