WATANZANIA wakiwemo vijana nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa za uwezeshaji wa mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri za wilaya , Manispaa na Majiji ili waanzishe miradi ya ujasiliamali ya kujikwamua na umaskini wa kipato.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 , Sahil Geraruma alitoa rai hiyo katika Kata ya Mazimbu Manispaa ya Morogoro baada ya Mwenge wa Uhuru kupitia kuona mradi wa kikundi cha vijana wa Chama cha Mafundi Ujenzi.
Geraruma alisema , Serikali ya awamu ya sita inawajali wananchi wake kwa kutoa fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo isiyo na riba kwa makundi ya vijana , wanawake na watu wenye ulemavu kupitia fedha zinazotolewa na Halmashauri za wilaya, Manispaa na Majiji.
“ Kwanza kabisa naomba niwafikishie habari njema vijana , kuna asilimia 10 zinazotokana na makusanyo ya fedha za ndani za Halmashauri na asilimia hiyo imegawanyika makundi matatu asilimia nne kwa vijana umri kuanzia miaka 18 hadi 35 “ alisema Geraruma
Alisema wanachopaswa ni kufuata utaratibu wa kuunda vikundi , kusajili kikundi , kuunda katiba ya kikundi kwa kuzingatia sheria ndogo ndani ya Halmashauri husika , kufuata taratibu zote kwenye Ofisi ya Maendeleo ya Jamii na ya mkurugenzi mtendaji na kwamba mkopo huo hauna riba.
Geraruma alitaja kundi lingine la wanawake ambalo lina asilimia nne na kwamba utaratibu ni kuunda vikundi vya watu kuanzia watano na kuwekewa ukomo wa umri ni kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Kundi lingine linalonufaika na mkopo huo ni la watu wenye ulemavu ambalo limetengewa asilimia mbili pia kwa utaratibu wa kuunda vikundi lakini wao hata mtu mmoja mmoja anaweza kukopeshwa.
“ Kwa hiyo ndugu zangu Rais ametoa fursa tuweza kunufaika nayo , watanzania wenzangu zingatieni fursa hiyo ili tuweze kunufaika , tusikae mitaani tukaanza kulalamika kila wakati maisha magumu ..maisha magumu wakati kuna fursa Rais ametoa na hatujazitumia “ alisema Geraruma
Aliwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa kupata mikopo isiyo na riba ili iwawezeshe kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zitawasaidia kuboresha maisha yao na pia kukuza uchumi wa Taifa .
Pamoja na hayo aliwataka wanufaika mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili endelee kutolewa kwa wezao mwengine na kwamba endapo kutajitokeza changamoto za kuchelewa kurejesha wanapaswa kuwasiliana na viongozi wa ngazi ya Halmashauri kutatua changamoto hizo.
Geraruma pia alitumia fursa hiyo kuipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kupitia Mkurugenzi wake kutenga fedha za asilimia 10 zitokanazo na mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake , vijana na watu wenye ulemavu.
Awali Katibu wa Kikundi cha vijana wa Chama cha Mafunzi Ujenzi , Annastazia Charles akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa mbio cha Mwenge wa Uhuru alisema kikundi kilianzishwa mwaka 2018 kikiwa na wanachama 11 ambapo wavulana ni tisa na wasichana wawili na kilipata usajili wa Manispaa mwaka 2020.
“ Kikundi hiki kinajishughulisha na kufyatua matofali mchanganyiko wa saruji na mchanga (blocks) kwa kutumia mtambo wa kushindilia mchanga na saruji” alisema Annastazia
Alisema mwaka 2021/2022 kikundi kilipata mkopo wa Sh milioni 24 ikiwa ni sehemu ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Manispaa kwa makundi ya ( wanawake, vijana na watu wenye ulemavu )na fedha hizo zilitumika kununua mashine mbalimbali na vifaa vya kufyatua matofali katika mradi huo .
Annastazia alisema hasi sasa mradi huo una thamani ya Sh milioni 39.2 ambazo Sh milioni 24 ni mkopo kutoka Halmashauri ya Manispaa hiyo na Sh milioni 15.2 ni mchango wa wanachama ukiwa ni mtaji wa kikundi chenyewe na mradi umekamilika na unatoa huduma.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa